Kiiza |
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza na beki
mzalendo, Juma Abdul wako hatarini kuukosa mchezo wa keshokutwa wa kirafiki wa
timu yao, dhidi ya timu ‘tishio’ kutoka Afrika Kusini, Black Leopard kutokana
na kuwa wagonjwa.
Wawili hao wanasumbuliwa na Malaria na leo wameshindwa
kufanya mazoezi na wenzao kujiandaa na mchezo huo unaotarajiwa kuwa ‘mkali na
wa kusisimua’.
Mabingwa hao wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC ya
Dar es Salaam Jumamosi hii watashuka kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam
kumenyana na Black Leopard ya Polokwane, Limpopo nchini Afrika Kusini.
Yanga ilikuwa Uturuki kwa wiki mbili kwa kambi ya mazoezi na
ilirejea Jumapili Alfajiri nchini. Katika ziara yake hiyo, ilicheza mechi tatu
za kujipima nguvu na kufungwa mbili na kutoka sare moja.
Katika mchezo wake wa kwanza, ilitoka sare ya 1-1 Ariminia
Bielefeld ya Daraja la Tatu (sawa na la nne) Ujerumani kabla ya kufungwa 2-1 na
Denizlispor FC ya Daraja la Kwanza Uturuki na baadaye 2-0 na Emmen FC ya Ligi
Daraja la Kwanza Uholanzi.
Yanga iliweka kambi katika hoteli ya Fame Residence Lara
& Spa kilomita chahce kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Jiji la Antalya, iliyopo
ufukweni mwa bahari ya Mediteranian.
Kikosi cha wachezaji 27 kilikuwa kambini nchini Uturuki, ambacho
ni makipa; Ally Mustafa 'Barthez', Said Mohamed na Yussuf Abdul, mabeki Juma
Abdul, Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Stefano Mwasyika, Oscar Joshua, Mbuyu
Twite, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Ladisalus Mbogo na Kelvin Yondani.
Viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Haruna
Niyonzima, Kabange Twite, Nurdin Bakari, Omega Seme, Simon Msuva, Rehani
Kibingu, Nizar Khalfani na David Luhende wakati washambuliaji ni Didier
Kavumbagu, Said Bahanunzi, Jerry Tegete, George Banda na Hamisi Kiiza na Kocha
Mkuu Mholanzi, Ernie Brandts, Kocha Msaidizi, Freddy Felix Minziro na Kocha wa
makipa na Razak Ssiwa.
Hiyo inakuwa mara ya tatu kihistoria Yanga kufanya ziara nje
ya Afrika baada ya Brazil mwaka 1975 na Romania mwaka 1978. Yanga pia imewahi
kuweka kambi Afrika Kusini mwaka 2008.
Leopards ilirejea Ligi Kuu ya Afrika Kusini mwaka juzi tangu
ishuke 2008 na msimu uliopita iliponea chupuchupu kushuka tena, baada ya
kushika nafasi ya 14 katika Ligi ya timu 16, na kwa msimu huu hadi sasa ipo
nafasi ya 12.
Katika mechi 15 zilizopita za klabu ya Black Leopard, imemudu
kushinda mechi mbili tu, nyingine zote imefungwa na kutoka sare.
No comments:
Post a Comment