Thursday, January 10, 2013

KIUNGO MTALAAMU WA AZAM AMBAYE ALIWAHENYESHA AKINA DROGBA KATIKA DIMBA LA TAIFA KWA MARA YA KWANZA ABDUHALIM HUMUD GAUCHO AONGEZA NGUVU AZAM VISIWAN ZANZIBAR,NA PAZI ATOLEWA KWA MKOPO JESHINI


KIUNGO mshambuliaji wa mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC, Zahor Iddi Pazi ametolewa kwa mkopo katika klabu ya JKT Ruvu Pwani.
Kutolewa kwa mkopo kwa Zahor, mtoto wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Iddi Pazi ‘Father’ kunafuatia kusajiliwa kwa wachezaji kadhaa wapya Azam katika dirisha dogo.
Miongoni mwa waliosajiliwa ni Humphrey Mieno, Joackins Atudo kutoka Kenya, Brian Umony kutoka Uganda na David Mwantika kutoka Prisons ya Mbeya.
Zahor licha ya kuwa mchezaji mzuri amekuwa hana bahati ndani ya kikosi chs Azam tangu asajiliwe msimu uliopita.
Mwanzoni mwa msimu, Zahor aliomba kwenda kucheza kwa mkopo Coastal Union ya Tanga, lakini uongozi wa klabu hiyo ukamkatalia.
Katika hatua nyingine, kiungo Abdulhalim Humud aliyekuwa majeruhi tangu Novemba mwaka jana, amejiunga na kikosi cha timu hiyo kilichopo Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi.
Humud ambaye mashabiki wake humuita Gaucho, wakimfananisha na Mwanasoka Bora wa Zamani wa Dunia, Mbrazil Ronaldinho Gaucho aliwasili Zanzibar jana, ingawa haijulikani kama atashiriki hatua iliyobaki ya Kombe la Mapinduzu au la.
Azam jana iliingia Fainali ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kuifunga Simba SC kwa penalti 5-4, kufuatia sare ya kufungana mabao 2-2 ndani ya dakika 120 usiku huu kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani hapa.
Hadi mapumziko, Azam FC walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na kiungo Mkenya, Humphrey Mieno dakika ya 10, akiunganisha kwa kichwa kona maridadi iliyochongwa na kiungo mzalendo, Ibrahim Mwaipopo.
Azam ilishambulia zaidi baada ya bao hilo, kabla ya Simba kuzinduka dakika tatu baadaye na kuanza kushambulia pia.
Mchezo huo ulisimama kwa dakika tano kuanzia ya 14 hadi 19 kutokana na umeme kukatika uwanjani hapo, hali iliyolazimisha kuwashwa kwa Jenereta.
Kipindi cha pili Simba walibadilika mno kiuchezaji na kuanza kutawala mchezo jambo ambalo liliwasaidia kupata bao la kusawazisha dakika ya 78, ambalo lilifungwa na Rashid Ismail.
Simba ilipoteza nafasi mbili za wazi za kufunga mabao ndani ya dakika 45 za kipindi cha pili na mchezo ukamalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1.
Katika dakika 30 za nyongeza, Simba walifanikiwa kupata bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 110, mfungaji Miraj Madenge.
Azam walionekana kupagawa baada ya kupigwa bao la pili na kuanza kucheza rafu za ovyo na kutoa maneno machafu kwa refa, jambo ambalo liliwaponza kupoteza wachezaji wawili ndani ya dakika mbili.
Refa Waziri Shekha alianza kumtoa nje kwa kadi nyekundu kiungo Mwaipopo dakika ya 114 na baadaye Jabir Aziz dakika ya 116. 
Wakati refa huyo akijiandaa kupuliza kipyenga cha kuhitimisha mchezo na mashabiki wa Simba wakiwa wameuteka Uwanja wa Amaan kwa shangwe zao, beki Emily Mgeta alimuangusha kwenye eneo la hatari beki Malika Ndeule na hivyo kuwa adhabu ya penalti.
Beki Mkenya, Joackins Atudo ambaye amekuwa akipewa dhamana ya kupiga penalti kwa sasa Azam FC, alikwenda kupiga mkwaju huo na kuukwamisha nyavuni kuwapatia Watoto wa Bakhresa bao la kusawazisha.
Kutoka hapo, mchezo ulihamia kwenye mikwaju ya penalti na usiku huo bahati haikuwa yake kiungo matata chipukizi wa Simba, Haroun Athumani Chanongo, kwani pamoja na kupiga penalti nzuri iliyokuwa ya pili kwa timu yake, iligonga mwamba wa juu katikati na kudunda chini kisha kurejea uwanjani.
Wachezaji wa Simba waliofunga penalti zao jana ni Komabil Keita ya kwanza, Jonas Mkude ya tatu, Miraj Adam ya nne na Ramadhani Mkiparamoto ya tano, wakati wa Azam waliofunga ni Gaudence Mwaikimba ya kwanza, Himid Mao ya pili, Atudo ya tatu, Samir Hajji Nuhu ya nne na Malika Ndeule ya tano.
Kwa matokeo hayo sasa, Azam itamenyana na mshindi wa mechi ya leo kati ya Tusker na Miembeni katika fainali Jumamosi.

No comments:

Post a Comment