Sunday, January 6, 2013

KIPRE TCHETCHE AAGA MAPEMA KOMBE LA MAPINDUZI 2013


Kipre Herman Tchetche akiwa jukwaani jana. Mguu wa kushoto amefunga bandeji, hiyo ndiyo sehemu iliyomtoa mapema kwenye Kombe la Mapinduzi mwaka huu

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Kipre Herman Tchetche hatacheza tena michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani hapa baada ya kuumia katika mchezo wa kwanza dhidi ya Coastal Union ya Tanga juzi.
Akizungumza  jana Uwanja wa Amaan, Tchetche alisema kwamba maumivu aliyoyapata ni makubwa chini ya kikanyagio kwa nyuma na atatakiwa kuwa nje kwa muda usiopungua wiki mbili akipata tiba.
“Sitacheza tena haya mashindano, maumivu yataniweka nje muda wote, ndio mambo ya soka, lakini namuomba Mungu nipone haraka nirudi kuitumikia klabu yangu,”alisema nyota huyo kutoka Ivory Coast.
Tchetche alikosa mchezo wa kwanza wa Azam jana, ilipoichapa Miembeni ya hapa mabao 3-1 na kufufua matumaini ya kutetea Kombe la Mapinduzi.
Matokeo hayo, yanaifanya Azam ifikisha pointi nne na kupanda kileleni mwa Kundi B, ikifuatiwa na Miembeni yenye pointi tatu, Coastal Union ya Tanga pointi mbili na Mtibwa Sugar yenye pointi moja inashika mkia.
Hadi mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa mabao 2-1. Azam walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya pili lililofungwa na beki Mkenya, Joackins Atudo akiunganisha kwa kichwa kona ya kiungo Mkenya, Humphrey Mieno.
Miembeni walisawazisha bao hilo dakika mbili tu baadaye, baada ya kona iliyochongwa na Adeyoum Saleh kuingia moja kwa moja nyavuni, kutokana na jitihada za mshambuliaji mkongwe, Monja Liseki kumbana kipa Mwadini Ally asiufikie mpira.
Baada ya bao hilo, Azam walicharuka na kuzidisha kasi ya mashambulizi langoni mwa Miembeni, jambo ambalo liliwasaidia kupata bao la pili dakika ya 34 baada ya mshambuliaji Gaudence Mwaikimba kuinasa pasi maridadi ya Mieno na kusogea nayo mbele kidogo kabla ya kumchambua kipa Suleiman Hamad.
Baada ya refa Ally Omar Kisaka kupuliza kipyenga cha kuashiria kutimu kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, makocha wa timu zote, Muingereza Stewaert Hall wa Azam na Salum Bausi walimfuata mwamuzi huyo kumzonga kwa madai ya kuchezeha ovyo.
Kipindi cha pili, refa huyo aliporejea kabla ya kuanzisha mchezo, aliwapa kadi nyekundu makocha wote.
Ikiongozwa na Kocha Msaidizi, Muingereza Kali Ongala, Azam ilipata bao lake la tatu dakika ya 87, mfungaji Uhuru Suleiman aliyeuwahi mpira uliorudishwa na beki kufuatia Gaudence Mwaikimba kutaka kufunga kwa kichwa.
Katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Samir Hajji Nuhu, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Salum Abubakar/Jabir Aziz dk 82, Humphrey Mieno/Ibrahim Mwaipopo dk 83, Gaudence Mwaikimba, Brian Umony/Abdallah Seif dk60 na Hamisi Mcha ‘Vialli’/Uhuru Seleman dk 65.
Miembeni FC; Suleiman Hamad, Mfaume Odello, Adeyoum Saleh, Salum Hajji, Salum Juma, Sabri Ally/Adam Hamisi dk 70, Laurent Mugiya, Suleiman Hajji, Monja Liseki/Mohamed Hamdan dk45, Rashid Roshwa/Peter Ilunda dk62 na Issa Othman.   
Katika mchezo wa kwanza, Coastal Union ya Tanga ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar ya Morogoro, katika mchezo wa Kundi B Kombe la Mapinduzi, jioni hii kwenye Uwanja wa Amaan visiwani hapa.
Hadi mapumziko, hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na Coastal Union ndio walitakiwa kujilaumu kwa kushindwa kutumia mwanya wa Mtibwa Sugar kucheza pungufu kutokana na beki wake, Salum Swedi kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 43.
Timu zilishambuliana kwa zamu katika kipindi hicho, upande wa Coastal ukiongozwa na Danny Lyanga na Mtibwa Hussein Javu.
Baada ya Swedi kutolewa nje kwa kadi nyekundu, kocha Mecky Mexime alimuinua beki Rajab Mohamed kwenda kuchukua nafasi ya mshambuliaji, Hassan Seif.
Kipindi cha pili, Mtibwa walirudi kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 58, mfungaji Ally Mohamed ‘Gaucho’ aliyepiga shuti la umbali wa mita 19 na kumtungua Juma Mpongo.
Coastal Union ilisawazisha bao hilo dakika ya 81, mfungaji Jerry Santo aliyefumua shuti la chini la umbali wa mita 24 na kumtungua kipa Hussein Sharrif.
Katika mchezo huo, kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa; Hussein Sharrif, Hamisi Issa, Yussuf Nguya, Salvatory Ntebe, Salum Swedi, Babu Ally Seif, Ally Mohamed ‘Gaucho’, Rashid Gumbo, Hussein Javu, Hassan Seif/Rajab Mohamed dk43 na Vincent Barnabas.
Coastal Union; Juma Mpongo, Ismail Khamis, Othman Tamim, Philip Metusela, Mbwana Khamis ‘Kibacha’, Hamisi Shengo, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Jerry Santo, Mohamed Miraj, Mohamed Soud Othman na Danny Lyanga.

No comments:

Post a Comment