Saturday, January 5, 2013

JUMA KASEJA NA MRISHO NGASSA WAONDOLEWA MAPINDUZI CUP





Uongozi wa klabu ya Simba umewaondoa kwenye kikosi cha timu hiyo kinachoshiriki mashindano ya kombe la mapinduzi, Juma Kaseja aliyeomba kupumzika na Mrisho Ngasa kutokana na kuwa majeruhi.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, amesema kuwa wamewatoa wachezaji hao kwenye mashindano haya kutokana na kuwa majeruhi.

"Kaseja na Ngasa hawatakuwepo kabisa kwenye mashindano ya Mapinduzi kwa sababu ni majeruhi na pia Kaseja aliomba kupumzika na uongozi umeliangalia hilo na kuamua kuwaondoa kikosini," .


Aidha, amesema kuwa benchi la ufundi limekubaliana na maamuzi hayo ya kuwaondoa kwenye kikosi kinachoshiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi yaliyoanza wiki hii mjini Zanzibar.


Awali, Kaseja aliuandikia barua uongozi wa timu hiyo kuomba kupewa miezi mitatu ya kupumzika kutokana na kucheza michezo mingi mfululizo akiwa na klabu yake hiyo pamoja na kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars'.


Simba kwa sasa inashiriki mashindano ya Mapinduzi ambapo Meneja wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo alisema kuwa mashindano yataisaidia timu yake kujiweka sawa kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania bara.


Alisema kuwa Simba ina wachezaji wengi chipukizi hivyo michuano hiyo ya kombe la mapinduzi itawapa nafasi kuonyesha uwezo wao.


Awali kulikuwa na taarifa kuwa kikosi cha timu hiyo kitaenda kuweka kambi nchini Oman kujiandaa na mzunguko wa pili lakini ushiriki wao katika michuano hiyo ya kombe la Mapinduzi ni wazi huenda safari hiyo isiwepo kwa kuwa mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania bara umepangwa kuanza Januari 19 mwaka huu.


Wakati Simba wakishiriki katika michuano hiyo, watani wao, Yanga wenyewe wapo nchini Uturuki walipokwenda kuweka kambi kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu.

No comments:

Post a Comment