Sunday, January 13, 2013

CHANETA KUADHIBU MIKOA AMBAYO HAIJAFANYA UCHAGUZI


Chama cha netiboli nchini (CHANETA) kimesema kitatoa adhabu kwa viongozi wa mikoa ambayo haijaitisha uchaguzi wa viongozi bila ya kutoa sababu za msingi.

Kaimu Katibu Mkuu wa CHANETA, Rose Mkisi amesema mikoa hiyo tayari viongozi wake wamemaliza muda wao lakini wanashindwa kuitisha uchaguzi wa viongozi.

Mkisi aliitaja mikoa hiyo ambayo iko hatarini kupewa adhabu na CHANETA ni pamoja na Tanga, Manyara, Arusha,Kilimanjaro Mara, na Rukwa.

Mikoa mingine ambayo bado haijaitisha chaguzi zake ni pamoja na Dodoma, Tabora, Shinyanga, Iringa,Kagera, na Kigoma.

 "Tunaomba mikoa hiyo ifanye chaguzi ili kufanikisha CHANETA kuitisha uchaguzi mkuu, bila ya kufanya hivyo itapewa adhabu," aliongeza  Mkisi.

 Mkisi aliongeza  mikoa hiyo ndio chanzo kikubwa cha CHANETA kuchelewa kuitisha uchaguzi mkuu kwa ajili ya kupata viongozi wapya watakaokiongoza chama hicho kwa muda wa miaka minne.

Mkisi aliitaja mikoa ambayo tayari imefanya chaguzi zake ni kuwa ni pamoja na Dar es Salaam, Mwanza, Lindi, Mtwara,Morogoro, Ruvuma, Mbeya, na Singida.

Alisema wakitekeleza zoezi hilo mapema itakuwa rahisi kwa CHANETA kuanza harakati za uchaguzi mkuu wa kuwapata viongozi wapya wa chama hicho.

Wakati huo huo, Mkisi aliwataka wachezaji wa timu ya taifa ya netiboli kujitokeza mazoezini kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya kimataifa yaliyopo kwenye kalenda ya mwaka.

 mazoezi hayo kwa sasa yatakuwa yanakwenda na kurudi nyumbani chini ya makocha Mary Protasi na Mary Waya kwa ajili ya kuiandaa timu hiyo na mashindano ya kimataifa yaliyopo kwenye kalenda ya mwaka. Aliongeza  wachezaji wote wanatakiwa kuhudhuria mazoezi hayo ili iwe rahisi kwa kocha kuweza kuchagua kikosi cha kwanza cha timu hiyo kitakachoiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment