Thursday, January 3, 2013

BABBI KUKIMBIA BENCHI AZAM, HUENDA AKAREJEA MTIBWA


Abdi Kassim
ABDI Kassim Sadallah ‘Babbi’ au Ballack wa Unguja yuko mbioni kuihama klabu ya Azam FC na kurejea na Mtibwa Sugar ya Morogoro, kutokana na kushindwa kuvumilia kuwekwa benchi chini ya kocha Muingereza, Stewart Hall.
  Babbi tayari yupo kwenye mazungumzo na Mtibwa Sugar, klabu yake ya kwanza kuchezea Tanzania Bara, ambayo imeonyesha nia ya kumpokea tena.
Babbi amekuwa akilalamika kwa watu wake wa karibu kwamba, wakati wa kocha Mserbia Boris Bunjak alikuwa anapangwa Azam na kufanya vizuri kiasi cha kuisaidia sana timu, lakini baada ya kurejea Stewart amekuwa mtu wa benchi.
Babbi amekuwa akisema Azam ilipokuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwezi uliopita kwenye Kombe la Hisani, alipangwa katika mechi mbili za mwanzo ambazo Stewart alibaki Kenya kwa kukosa viza ya kuingia Kinshasa.
Amekuwa akilalamika kwamba pamoja na kucheza vizuri katika mechi hizo, maisha yalibadilika ghafla baada ya Stewart kutua Kinshasa, kwani kuanzia hapo hakumbuki kama alivaa tena hata jezi ya Azam hadi mashindano yanaisha.
Habari zaidi zinasema, tayari Babbi amekwishawaeleza nia yake ya kuondoka baadhi ya viongozi wa Azam, ambao wameonekana kukosa namna ya kumzuia, kwa sababu nao wanaona ana sababu ya kufikia uamuzi huo, kunusuru kiwango chake.   
Azam ipo visiwani hapa kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi, lakini katika mchezo wa jana dhidi ya Coastal Union alikuwa sehemu ya watazamaji jukwaani.

No comments:

Post a Comment