Friday, January 18, 2013

AUSTRALIA OPEN: SHARAPOVA AMUONDOSHA VENUS WILLIAMS.


Mchezaji tenisi nyota anayeshika namba mbili katika orodha za ubora duniani kwa upande wanawake, Maria Sharapova amefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora katika michuano ya wazi ya Australia inayoendelea jijini Melbourne baada ya kumfunga Venus Williams. Sharapova mwenye umri wa miaka 25 raia wa Urusi alimfunga Williams ambaye ni bingwa mara saba wa mataji ya Grand Slam kwa 6-1 6-3 akitumia muda wa dakika 76 ambapo sasa anatarajia kukutana na Kirsten Flipkens wa Ubelgiji katika hatua inayofuata. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Sharapova amesema alikuwa amejiandaa vya kutosha kwakuwa alikuwa akijua mchezaji ambaye anakutana naye. Mwanadada huyo aliendelea kusema pamoja na Williams kuporomoka katika viwango vya ubora mpaka nafasi ya 24 lakini alijua kuwa ana uzoefu wa kutosha wa mashindano hayo na lolote lingeweza kutokea. Williams mwenye umri wa miaka 32 ambaye alikaa nje kwa kipindi cha miezi saba baada ya kusumbuliwa na maradhi ya ngozi alimsifu mpinzani kwa kucheza vizuri na kutumia vyema makosa mengi aliyokuwa akiyafanya kwenye mchezo huo.

No comments:

Post a Comment