Tuesday, January 8, 2013

ARMINIA ILIYOTOKA 1-1 NA YANGA NI YA DARAJA LA NNE UJERUMANI, WAPINZANI WA LEO KWELI DARAJA LA KWANZA


Yanga SC

YANGA SC ipo Uturuki kwa ziara ya wiki mbili na Jumamosi iliyopita ilicheza mechi ya kwanza ya kujipima nguvu na klabu ya DSC Arminia Bielefeld, au Deutscher Sportclub Arminia Bielefeld kwa jina kamili inayojulikana pia kama Die Arminen au Die Blauen.
Hii ni klabu ya soka kutoka mji wa Bielefeld, North Rhine-Westphalia, yenye wanachama  8,738 inayotumia jezi za rangi nyeusi, nyeupe na bluu na inacheza Ligi Daraja la Nne Ujerumani, inayoitwa 3. Liga, na msimu uliopita ilishika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi inayoshirikisha timu 18.
Imewahi kupanda na kushuka Ligi Kuu ya Ujerumani, maarufu kama Bundesliga, mara saba, ambayo kwa Ujerumani ni rekodi. Mwaka 1971 ilikumbwa na kashfa ya kuwahonga wapinzani wao katika Bundesliga.
Arminia imekuwa ikicheza mechi zake za nyumbani katika Uwanja wa Bielefelder Alm tangu mwaka 1926 na kuanzia mwaka 2004, Uwanja huo umekuwa ukiitwa SchucoArena, kutokana na dili la udhamini walilopata.
KUHUSU LIGI WANAYOCHEZA;
3. Fußball-Liga ni Ligi Daraja la Nne Ujerumani, ambayo ilianza kuchezwa msimu wa 2008–2009, ikichukua nafasi ya Regionalliga kama ligi ya nne kwa ukubwa Ujerumani.
Katika mfumo wa ligi za soka Ujerumani, inatenganishwa na 2. Bundesliga na Semi-Professional Regionalliga, hivyo inakuwa kama Daraja la Nne na huchezwa katika makundi matatu, yenye jumla ya klabu 18 zilizogawanywa katika makundi hayo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Yanga, timu hizo zilitoka sare ya 1-1 Jumamosi.
WAPINZANI WA LEO KWELI DARAJA LA KWANZA;
Leo Yanga inacheza mechi ya pili ya kujipima nguvu dhidi ya timu ya Denizlispor FC yenye maskani yake Denizli, nchini Uturuki, ambayo kweli inashiriki Ligi Daraja la Kwanza, iitwayo Bank Asya 1. Lig na msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya 10.
Denizlispor Football iliyoanzishwa mwaka 1966, inatumia Uwanja wenye kuingiza mashabiki 19,500 wa Denzili Ataturk na mafanikio yake makubwa hivi karibuni ilikuwa mwaka 2002 waliposhika nafasi ya tano katika Ligi Kuu ya nchini humo na kufuzu kwenye mchujo wa Kombe la UEFA.
Mwaka huo, ilifanya maajabu kwa kuzifunga timu zenye majina Ulaya kama FC Lorient, Sparta Prague na Olympique Lyonnais, kabla ya kufungwa katika Raundi ya Nne na FC Porto ya Ureno, ambao walitwaa ubingwa wa michuano hiyo mwishowe.  Je, matokeo yatakuwaje kwenye mechi hiyo leo?

No comments:

Post a Comment