Tuesday, January 8, 2013

WAWILI TU YANGA KUJIUNGA NA STARS ITAKAYOMENYANA NA ETHIOPIA


Domayo
WACHEZAJI wawili tu wa Yanga, beki Kevin Yondan na kiungo Frank Domayo ndio watajiunga na kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinachotarajiwa kuondoka kesho mchana kwenda Ethiopia, imeelezwa.
Yanga ambayo imepiga kambi ya maandalizi nchini Uturuki ilizuia nyota wake kujiunga na kambi ya Stars iliyoanza jumapili iliyopita jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa keshokutwa katika uwanja wa Taifa wa Addis Ababa.
Akizungumza leo mjini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kwamba Kocha Mkuu wa Stars, Mdenmark Kim Poulsen na Mholanzi Ernie Brandts wa Yanga, wamekubaliana Yondan na Domayo pekee, kati ya wachezaji watano Yanga waliotwa Stars ndio wajiunge na timu hiyo.
Amesema wachezaji hao wanatarajiwa kuwasili nchini usiku wa leo tayari kwa safari kesho na endapo watachelewa watakwenda Ethiopia peke yao, huku wachezaji wengine wa Yanga walioitwa Stars ambao wataendelea kubaki nchini Uturuki ni pamoja na Athuman Iddy ‘Chuji’, Simon Msuva na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ watakaojiunga na Stars watakaporejea nchini Januari 13.
Wambura aliongeza kuwa wachezaji 16 wa Stars wataondoka kesho saa 9:00 Alasiri tayari kwa mchezo huo maalum kwa kuipa maandalizi ya mwisho Ethiopia kabla ya kwenda Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazoanza Januari 19 mwaka huu.
Aidha, Wambura aliongeza kuwa, tayari wachezaji wa Simba, Azam FC na Mtibwa Sugar waliokuwa Zanzibar na timu zao zinazoshiriki michuano ya kombe la Mapinduzi inayoendelea Visiwani Zanzibar wamewasili leo kuungana na wenzao.
“Hata hivyo Azam  Fc imeruhusu kipa mmoja tu Aishi Manula huku Mwadini Ally ambaye pia aliitwa Stars ataendelea kubaki na timu kwenye kombe la Mapinduzi,”alisema Wambura
Wambura aliongeza kuwa kikosi cha Stars kilichoanza rasmi mazoezi jana, leo asubuhi kilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume na jioni kinatarajiwa kujinoa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Aliwataja wengine wachezaji waliopo ni pamoja na Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha wa Stars na  Manula ( Azam FC), huku kwa upande wa Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), wakati washambuliaji ni Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu  (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na  Mrisho Ngasa (Simba).
Stars ambayo pia itautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya mechi ya mchujo dhidi ya Morocco kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014, mchezo utakaochezwa Machi mwaka huu.
Katika maandalizi yake hayo, mara ya mwisho  Stars ilikwaana na Zambia Desembza 22 mwaka jana kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na  kuibanjua bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki

No comments:

Post a Comment