Thursday, October 11, 2012

YANGA YAZINDUKA, YALICHARAZA TOTO LAKE TOVU LA ADABU BAKORA ZA KUTOSHA

Kavumbangu; Mfungaji wa bao la kwanza la Yanga
 (Picha na Maktaba ya BIN ZUBEIRY)


YANGA SC leo imezinduka baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Toto African, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
 
Matokeo haya, yanaifanya Yanga itimize pointi 11, katika mechi saba ilizocheza hadi sasa, ikiwa imefungwa mbili, sare mbili na kushinda tatu, inazidiwa pointi tano na wapinzani wake wa jadi, Simba SC wanaoongoza ligi hiyo kwa pointi zao 16, wakifuatiwa na Azam wenye pointi 13.
 
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-0, yaliyopachikwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu na beki wa kimataifa wa Rwanda, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbuyu Twite.
 
 
Kavumbangu alifunga bao la kwanza dakika ya pili, baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Erick Ngwengwe kufuatia kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima, hilo likiwa bao lake la tano ndani ya mechi 11 tangu ajiunge na Yanga msimu huu akitokea Atletico ya kwao, Burundi.
 
 
Baada ya bao hilo, Yanga waliendelea kulisakama lango la Toto na dakika ya 21, Mbuyu Twite akaunganisha kona ya chini chini iliyochongwa na Niyonzima.
 
 
Toto ilipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 42, baada ya kupata penalti, kufuatia beki mmoja wa Yanga kuunawa mpira kwenye eneo la hatari, baada ya Wana Kishamapanda kufanya shambulizi kali la kushitukiza, lakini kiungo Emanuel Swita akapiga nje.
 
 
Swita alipiga penalti nzuri tu ya chini pembeni kabisa, lakini vipimo vyake vikazidi kidogo, mpira ukatoka nje, ingawa Berko aliifuata vizuri pembeni kabisa kulia kwake na angeweza kuokoa.
 
 
Kipindi cha pili Toto waliingia kwa kasi zaidi na kuanza kulishambulia lango la Yanga mfululizo, wakitawala zaidi sehemu ya kiungo.
 
 
Katika dakika ya 54 mshambuliaji Mussa Said aliifungia Toto bao safi, baada ya kipa Yaw Berko kutoka langoni.
 
 
Baada ya bao hilo, Toto walizidi kutawala mchezo na kukosa mabao mawili ya wazi- hapo ndipo kocha Mholanzi, Ernie Brandts akawatoa viungo Frank Domayo na Athumani Idii ‘Chuji’ na kuwaingiza Shamte Ally na David Luhende.
 
 
Walipoingia Shamte na Luhende wote walienda kushambulia pembeni na Haruna Niyonzima na Nurdin Bakari wakarudi katikati.
 
 
Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga kupata bao la tatu dakika ya 68, lililofungwa kitaalamu na mshambuliaji Jerry Tegete ambaye alimpiga chenga kipa Ngwengwe baada ya kupokea pasi ya Oscar Joshua.  
 
 
Baada ya bao hilo, Kocha wa Toto, Johh Tegete naye alifanya mabadiliko akiwatoa Mussa Said na Evarist Maganga na kuwaingiza Heri Mohamed na Heri Kyaruzi. Hata hivyo, pamoja na mabadiliko hayo, Yanga waliendelea kutawala mchezo hadi filimbi ya mwisho.
 
 
Kwa ushindi huu, Yanga imelipa kisasi cha mara ya mwisho timu hizo, zilipokutana kwenye Uwanja huo, Jumapili ya Aprili 15, mwaka huu, Toto walipoibuka na ushindi wa mabao 3-2.
 
 
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Yaw Berko, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’/Shamte Ally, Frank Domayo/David Luhende, Haruna Niyonzima, Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Nurdin Bakari.
 
 
Toto; Erick Ngwengwe, Kulwa Greyson, Eric Mulilo, Evarist Maganga/Heri Kyaruzi, Peter Mabula, Hamisi Msafiri, Emanuel Swita, Haroun Athumani, Mohamed Hussein, Suleiman Kibuta na Mussa Said/Heri Mohamed.  

MFALME WA RAB BONGO KUANZA KUSAKWA JUMAPILI DAR LIVE

 

 

KIUNGO SIMBA APATA MAISHA MAPYA MALAYSIA

KIUNGO wa zamani wa Simba SC, Hillary Fordy Echesa kwa sasa anachezea klabu ya Muar FC ya Ligi Kuu ya Malaysia, yenye maskani yake mjini Muar, Johor, aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Tusker FC ya Kenya.
Klabu hiyo inatumia Uwanja wa Sultan Ibrahim uliopo Muar, Johor na Echesa ni tegemeo katika klabu hiyo. Hii inakuwa klabu ya 10 kwa Echesa tangu aanze soka ya ushindani mwaka 2001, alipoibukia Nzoia Sugar ya kwao, ambayo aliichezea hadi 2003 alipohamia Ulinzi Stars, ambayo aliichezea hadi 2005 alipohamia Mumias Sugar, zote za Kenya na mwaka 2006 akajiunga kwa muda na Yanga ya Dar es Salaam, ambayo iliachana naye akaenda Rayon Sport ya Rwanda mwaka 2006, alikocheza hadi 2008 akaenda Polis Di-Raja (PDRM FA) ya Malaysia, alikocheza msimu mmoja na kujiunga na Deltras aliyoichezea 2009 kabla ya kutua Simba SC mwaka 2010, ambayo baada ya msimu mmoja ilimtema akaenda Tusker ya kwao, Kenya aliyoichezea kwa msimu mmoja na sasa amerejea Malaysia.             

Echesa alipokuwa Simba SC 

Echesa akilima nyumbani kwake Nairobi

Echesa alipokuwa Simba

Echesa katika mazoezi ya ufukweni

Echesa katika mazoezi ya gym 

Echesa nyumbani

Echesa Malasyia
Wasifu wa Hillary Echesa
Personal information
JINA KAMILIHillary Echesa
KUZALIWASeptemba 9 1981 (Miaka 31)
PALIPOZALIWAKenya
UREFUFuti 5 na inchi 9 
NAFASIKiungo
KLABU ALIZOCHEZEA
KLABU YA SASAMP Muar FC
KLABU ZA AWALI
MwakaKlabu

2001-2003Nzoia Sugar

2003-2005Ulinzi Stars

2005-2006Mumias Sugar

2006Yanga

2006Rayon Sport

2006-2008PDRM FA

2008-2009Deltras

2010Simba

2011Tusker

2012MP Muar

TIMU ZA TAIFA
1997Kenya Kenya U-17

2000-2003Kenya Kenya U-23

2001-2009Kenya Kenya(Mechi 31, mabao6)

AFRICAN LYON WAMTOLEA UVIVU TENGA NA TFF YAKE

Msemaji wa African Lyon, Sherallu Abdallah (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari, katika hoteli ya New Avon leo. Kushoto ni Katibu wa Azam, Rahim Kangezi 'Zamunda' na kulia ni kocha Muargentina wa Lyon,Pablo Ignacio Velez . 

“Kwanza kabisa tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa makundi yafuatayo kutokana na kazi kubwa waliyofanya ya kutusaidia,kutupa moyo wakati tukukiwa katika wakati mgumu:
1. Viongozi wote wa klabu 14 na ushirikiano wao katika kutupa moyo wakati wa mapambano. Kitendo hicho kimeonyesha umoja tulionao na kukomaa katika uongozi wa soka nchini.
Ushirikiano huo umetuwezesha kupambana vilivyo katika kusaka maslahi ya timu pamoja na kusonga mbele katika suala udhamini pamoja na Vodacom kushindwa kufuatwa matakwa yetu. Hali hiyo inatupa moyo kuwa tunaweza kufanikia hapo baadaye.
Pamoja na TFF kushindwa kutoa msaada kwetu, klabu ziliweza kupambana vilivyo na kuweka mkazo mkubwa katika ligi.
2. Shukrani zetu za pili kwa vyombo vya habari na wachambuz mbali mbali wa mpira wa miguu. Vyombo vya habari vimeweza kufuatilia suala hilo kwa umakini mkubwa huku vikiuliza maswali ya msingi na kuonyesha jinsi gani TFF imekukuwa ikipotosha suala hili.
3. Pia tunaweza kutoa shukrani kubwa kwa mashabiki wa soka kwa kuonyesha sapiti kubwa na kuonyesha jinsi gani mpo bega kwa bega na klabu mbali ya kuupenda mchezo wa soka na maendeleo ya mchezo huo kwa
ujumla.
4. Shukrani zetu pia kwa Mdhamini wetu mkuu, Kampuni ya simu ya mkononi ya Zante kwa kuonyesha kuwa ni mdau wa kweli kwa asilimia 100 kwa kuonyesha nia ya dhati ya kuendeleza soka la vijana pamoja na vipingamizi mbali mbali, hata hivyo hawakukata tamaa na kuheshimu mkataba wetu.
5. Mashabiki na wadau wa African Lyon na uongozi. Tunawapa shukrani kubwa kwa kuwa karibu nasi kwa kutupa moyo wakati wa mtafaruku mkubwa na kutuhamasisha katika mapambano haya. Busara zao
zilituwezesha kufikia hatua hii ya leo.
Ndugu waandishi wa habari; Wiki kadhaa zilizopita kulikuwa na harakati za kuhakikisha kuwa kipngele cha Upekee katika udhamini “exclusivity” kichoibuka kabla ya kuanza kwa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Tupo mbele yenu kuweka kila kitu kuhusiana na suala hilo wazi na katika mstari kutokana na sababu suala hilo limepotoshwa na kuweka mtazamo hasi kwa klabu ya African Lyon.
Lengo letu la kwanza katika mkutano huu ni kusafisha jina la African Lyon na hasa kutokana na mtazamo wa wengi kuwa tatizo hilo limetokana na msimamo wa klabu yetu.
Ni jambo la kusikitisha na kutisha kuona kwamba chombo kilichopewa mamlaka makubwa ya kuendeleza mpira wa miguu nchini kuisukumizia lawama klabu ndogo kama wakati chanzo cha matatizo hayo yanetokana na utendaji wao.
Kama hatutaweza kutatua tatizo hili kwa sasa, hatutaweza kufikia muafaka hapo baadaye na linaweza kuzihusisha klabu kubwa na mapambano yatakuwa makubwa zaidi.
Yafuatayo ni vithibitisho au “fact” ambazo tunawaomba kutoa majibu:

1. Mkataba kati ya TFF na Vodacom Tanzania ulisainiwa Agosti 11, siku 4 kabla ya ligi kuanza
2. Klabu hazikuwa na taarifa kuwa mkataba umesainiwa na TFF panoja na ligi kuanza.
3. Klabu zilisisitiza kuwa mkataba unatakiwa kusainiwa angalau kuwahusisha wajumbe watatu kutoka vilabu vya ligi kuu, jambo ambalo halikufanyika.
4. Taarifa iliyotolewa na Rais wa TFF kuhusiana na kipengele cha Upekee “exclusivity” na kuwapa sapoti Vodacom ilikuwa na upotoshaji kwani kuondolewa kwa kipengele hicho si mara ya kwanza katika soka la
Afrika na Dunia kw ujumla. Mfano: Ligi ya Ghana inadhaminiwa na kampuni ya simu ya Glo Mobile Ghana amabpo timu ya Asante Kotoko inadhaminiwa na kampuni ya simu ya mkononi ya MTN Ghana. 
Huu ni mfano mmoja kwani kuna mifano mingi tu.
5. Vodacom haita ilipa fidia African Lyon kwa kufunjika kwa
mkataba wao na mdhamini kutokana na kipengele cha upekee.
6. TFF haitailipa fidia African Lyon kwa kukubali kipengele hicho katika hatua za mwisho kabla ya ligi kuanza.
7. Access to the contract for clubs to understand the clauses and issues involved is limited to going to TFF office and looking at the contract there.
8. Hakuna hata klabu moja inayofahamu kuhusiana na mkataba wa sasa ambao TFF inadai kuwa umepata Baraka zote kutoka kwa viongozi wa klabu za ligi kuu.
9. Mkataba ambao umesainiwa hivi karibuni unawapa nafasi Vodacom haki ya kukataa mapendekezo ya vilabu vya ligi kuu na kuzifanya klabu hizo kuwa katika wakati mgumu wa kupata mdhamini mwingine.
10. Fedha za udhamini zitolewazo na Vodacom hazitoshi kuendesha klabu kutokana na urefu wa lligi na masuala mingine.
African Lyon haiwezi kupingana na Vodacom kwa sababu mkataba ulisainiwa baina yao na TFF. Hata hivyo kisheria tuna kesi ngumu sana na TFF na tunapenda kuuliza maswali haya mawili na kupata majibu yake.
1. Wanatarajia klabu kuweka nguvu zao pembeni za kupata mdhamini mwingine mpaka TFF isaini mkataba na Vodacom ambao ulisainiwa siku nne kabla ya ligi kuanza?
2. Je mnaweza kuishusha daraja African Lyon kama itashindwa kwenda kucheza mechi za ligi mkaoni Kagera au Mbeya kutokana na kukosa fedha?
Instead of TFF making a case to the public that they unsuccessfully worked with clubs to try and remove the “exclusivity” clause, they are the ones making a case on behalf of Vodacom’s marketing department that the “exclusivity” clause should have been there. 
Why would you fight Vodacom’s battle with the public who clearly feel that the “clause” hurts the development of this game?
African Lyon inataka yafuatayo kutoka kwa TFF:
1. TFF lazima ikubali kuwa mtatizo haya ya mkataba yamesabaishwa na wao kutokana na kushindwa kufuata utaratibu uiowekwa na klabu na kusainiwa wao mkataba
2. TFF ikubali kuwa itaendeleza mkataba mpya wenye mabadiliko baada ya kumalizika kwa huu.
3. TFF ikutane na Zantel na kuwashukuru kwa kutojitoa katika majukumu yake na African Lyon,”

Sherally Abdallah
Msemaji African Lyon
Katibu wa Lyon, Zamunda akifafanua jambo wakati akizungumza na Waandishi leo
Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Lyon, Saya Lindsay akifuatilia mkutano

AZAM WAFUATA POINTI TATU MOROGORO LEO

Azam FC


AZAM FC inatarajiwa kuondoka leo mchana kwenda Morogoro, tayari kwa mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Polisi, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
 
 
Azam kwanza watafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chamazi asubuhi ya leo, na baada ya hapo watapanda basi lao, lenye kila kitu ndani- TV, friji, choo, mziki wa maana na siti za kulala kwa safari ya takriban saa mbili kwenda Mji Kasoro Bahari.
 
 
Azam imepania kushinda mechi hiyo Jumamosi ili kuiondoa Simba kileleni na kuzidi kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
 
Katika kujiandaa na mechi ya Morogoro, Azam juzi ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kufungwa na Simba SC mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
 
Mabao ya Simba juzi yalifungwa Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
 
Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya 2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
 
Azam na Simba zitakutana tena katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.     
 
Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.

HASIRA ZA YANGA KWA TOTO KIRUMBA LEO

Blandts kushoto akiwanoa wachezaji wake, leo watashinda Mwanza?


MABINGWA wa kihistoria wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC ya Dar es Salaam, leo wanashuka kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kumenyana na wenyeji Toto African, katika mchezo ambao wamepania kushinda ili kurejesha matumaini ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Yanga ambayo katika mechi sita ilizocheza hadi sasa, imefungwa mbili, sare mbili na kushinda mbili, inazidiwa pointi nane na wapinzani wake wa jadi, Simba SC wanaoongoza ligi hiyo kwa pointi zao 16, wakifuatiwa na Azam.
Msimu uliopita, Yanga iliambulia nafasi ya tatu katika Ligi Kuu na kukosa nafasi ya kucheza michuano ya Afrika, Simba walioibuka mabingwa wakijikatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa na washindi wa pili Azam watashiriki Kombe la Shikrikisho.
Na tayari sasa Yanga wameanza kuhofia hali hiyo kujirudia na msimu huu, hivyo wameamua kukaza uzi, ili kujihadhari na matokeo mabaya.
Baada ya kufungwa mechi iliyopita na Kagera Sugar mjini Bukoba, Yanga wamepania kushinda leo na inaelezwa hadi Mwenyekiti wake, Yussuf Mehboob Manji amekwenda Mwanza kuongeza morali ya wachezaji kwa ajili ya mechi hiyo.
Kihistoria, Toto ni tawi la Yanga pale Mwanza, lakini uhusiano wao unaonekana kuanza kuyumba, baada ya timu hiyo ya Kishamapanda kuwageuzia kibao baba zao msimu uliopita kwa kuwafunga katika mchezo ambao walihitaji kushinda ili kufukuzana na Simba na Azam.  
Tayari kuna imani ndani ya Yanga kwamba wapinzani wao, Simba SC ‘wanatia mkono’ mechi zao kwa kuzipa motisha timu wanazocheza nazo zicheze kwa nguvu na kwamba hiyo ndiyo inasababisha mechi zao zinakuwa ngumu msimu huu.
Na ni kwa sababu hiyo katika mchezo wa leo, matajiri wote wa Yanga watakuwapo kwenye Uwanja wa Kirumba kuhakikisha baada ya dakika 90 wanaondoka na pointi tatu.
Mechi ya leo itakuwa ya tatu Yanga inacheza chini ya kocha wake mpya, Ernie Blandts ambaye hadi sasa hajashinda hata mechi moja, akiwa ametoa sare moja na wapinzani wao wa jadi, Simba SC, kufungwa moja dhidi ya Kagera.
Katika mchezo wa leo, Yanga itawakosa wachezaji wake wanne wa kikosi cha kwanza, beki Kevin Yondan, mshambuliaji Said Bahanuzi ambao wote ni majeruhi waliomua katika mechi mbili zilizopita, mshambuliaji Hamisi Kiiza aliyerejea kwao Uganda kuchezea timu yake ya taifa na kiungo Simon Msuva anayetumikia adhabu ya kadi.
Yondan alikanyagwa na Haruna Moshi ‘Boban’ kwenye mechi dhidi ya Simba Jumatano iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na atakuwa nje kwa wiki mbili na ushei, wakati Bahanuzi aliumizwa na Benjamin Effe wa Kagera Jumatatu naye atakaa nje kwa wiki moja au zaidi.
Lakini bado Blandts, beki wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, aliyeng’ara kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978 ana wachezaji wengine wa ushindi, ambao anaweza kuwatumia leo.
Bila shaka, kikosi Yanga leo kitakuwa; Yaw Berko, Juma Abdul, Stefano Mwasyika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Nizar Khalfan, Didier Kavumbangu, Jerry Tegete na Haruna Niyonzima.
Katika mechi ya jana ya ligi hiyo, Kagera Sugar walilazimishwa sare ya bila kufungana na JKT Ruvu ya Pwani katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

No comments:

Post a Comment