Wednesday, October 24, 2012

YANGA YAZIDI KUNG'ARA LIGI KUU, AZAM YABANWA NA RUVU CHAMAZI

Msuva kulia akishangilia na wenzake baada ya kufunga bao la kwanza. Kushoto ni Jerry Tegete na David Luhende


YANGA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa Polisi Morogoro mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, unaifanya Yanga itimize pointi 17, baada ya kucheza mechi tisa na kuendelea kusimama katika nafasi ya tatu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 18, baada ya sare ya 1-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.   
Ruvu walipata bao lao kupitia kwa Seif Abdallah na Kipre Tcheche akaisawazishia Azam.
Uwanja wa Taifa, hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyotiwa kimiani na washambuliaji Simon Msuva na Didier Kavumbangu.
Msuva alikuwa wa kwanza kuwainua vitini mashabiki wa Yanga dakika ya tano kabla ya dakika moja baadaye, Mrundi Kavumbangu naye kuwapa raha mashabiki wa timu hiyo.
Yanga ingekwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa mabao 3-0 kama mkwaju wa penalti wa Haruna Niyonzima usingegonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya mabeki wa Polisi kuondosha kwenye hatari.
Refa Alex Mahagi kutoka Mwanza alitoa penalti hiyo, baada ya Msuva kuangushwa na beki John Bosco kwenye eneo la hatari wakati anakwenda kufunga.    
Kipindi cha pili Yanga walirudi kwa kasi tena na kuendelea kulishambulia lango la Polisi, ingawa walipoteza nafasi nyingi na kutumia moja tu, dakika ya 58, mfungaji Hamisi Kiiza aliyeingia kuchukua nafasi ya Jerry Tegete.
Katika mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Coastal Union iliifunga 1-0 African Lyon Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Mtibwa Sugar imelazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Matokeo ya leo yanaziweka karibu mno, Simba, Azam na Yanga pale juu, kiasi kwamba ushindani na uhondo wa ligi hiyo unaongezeka.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Nahodha), Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Nurdin Bakari, Jerry Tegete/Hamisi Kiiza, Didier Kavumbangu na David Luhende/Nizar Khalfan.
Polisi; Manji Kulwa/Kondo Salum, Nahodha Bakari, John Bosco, Noel Msakwa, Salmin Kissi, Hamisi Mamiwa, Bantu Admin/Paul John, Paschal Maige, Mokili Rambo (Nahodha), Malimi Busungu na Nicholas Kabipe/Keneth Masumbuko.
Katika mchezo wa awali wa utangulizi, Yanga B imeifunga TMK United ya Ligi Daraja la Pili, mabao 6-1 katika mchezo wa utangulizi kabla ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kati ya Yanga na Polisi Morogoro.
Mabao ya Yanga yamefungwa na Georgeb Banda matatu katika dakika za 61, 70 na 72, Hussein Moshi dakika ya 12 na Rehani Rehani dakika ya 19 na 27, wakati la kufutia machozi la TMK United, lilifungwa na Abdi Hashimu dakika ya 62.

YANGA B 'WAITILIA UBANI' YANGA A TAIFA, WAPIGA MTU SITA

Yanga B imeifunga TMK United ya Ligi Daraja la Pili, mabao 6-1 katika mchezo wa utangulizi kabla ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kati ya Yanga na Polisi Morogoro. Mabao ya Yanga yamefungwa na Georgeb Banda matatu katika dakika za 61, 70 na 72, Hussein Moshi dakika ya 12 na Rehani Rehani dakika ya 19 na 27, wakati la kufutia machozi la TMK United, lilifungwa na Abdi Hashimu dakika ya 62. Tazama picha za mechi.
Abdulrahman Ally kulia akienda kuutoa mpira nyavuni baada ya George banda kushoto kufunga bao la sita

Kikosi cha Yanga B

George Banda kulia anawafunga tela mabeki wa TMK United 

Mchezaji wa yanga B akimtoka beki wa TMK

Kocha Mkuu wa Yanga B, Salvatory Edward kulia akiwa na Msaidizi wake Abubakar Salum

Wachezaji wa Yanga A, Mbuyu Twite, Haruna Niyonzjma, Ally Bart6hez na Nadir cannavaro wakishuhudia wadogo zao wanavyotoa adhabu

Okwi wa Yanga akivaa jezi kuingia dakika 10 za mwisho

BOBAN, NYOSSO WASIMAMISHWA SIMBA SC


Boban
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KLABU ya soka ya Simba inapenda kutoa taarifa zifuatazo kwenu siku ya leo.
1.    Kuhusu Boban na Nyoso
Wachezaji wawili wa Simba, Haruna Moshi Shaaban (Boban) na Juma Said Halfan (Nyoso), wamesimamishwa kuitumikia timu ya wakubwa (senior) kwa sababu na nyakati tofauti.
Moshi amesimamishwa kuichezea timu ya wakubwa kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu na kutokuwa na heshima kwa mwajiri (timu). Klabu imempa Haruna muda wa siku 21 kutoa maelezo kuhusu makosa yake na iwapo atashindwa kutoa maelezo ya kuridhisha, klabu inaweza kumchukulia hatua zaidi.
Katika kipindi hicho (siku 21 kuanzia jana), Boban atapokea nusu ya mshahara wake wa kila mwezi na hatapata marupurupu yoyote yanayohusiana na timu ya wakubwa.
Kwa upande wa Nyoso, uongozi umemwagiza afanye mazoezi na kikosi cha timu ya pili (Simba B) hadi hapo atakapoimarisha kiwango chake cha uchezaji.
Hatua hii imetokana na ripoti ya benchi la ufundi iliyoonyesha kwamba mchezaji huyo amekuwa akifanya makosa mengi ya kiuchezaji yanayoigharimu na ingawa amekuwa akipewa maelekezo na walimu, bado amekuwa akirudia makosa yaleyale.
Kutokana na hilo, Nyoso atafanya mazoezi na wachezaji wa kikosi cha pili hadi walimu watakaporidhika kwamba amejirekebisha na yuko tayari kutumikia kikosi cha wakubwa.
Katika muda wake wote huo akifanya mazoezi na timu B, Nyoso atakuwa akipata mshahara wake wa kila mwezi kama kawaida na pia atapata marupurupu wanayopata wachezaji wa Simba B.

Emmanuel Okwi
Klabu ya Simba inaeleza kusikitishwa kwake na taarifa za vyombo vya habari vyenye lengo la kuuza magazeti pasipo kujali athari za habari zenyewe.
Kwa mfano, habari ya kwenye gazeti la CHAMPIONI la leo ina kichwa cha habari KATIBU MKUU AMFUKUZA OKWI SIMBA. Hata hivyo, kilichoandikwa ndani ya habari yenyewe kinamnukuu aliyewahi kuwa Katibu Mkuu kwenye miaka ya nyuma.
Gazeti hilo linafahamu kabisa kwamba Simba ina Katibu Mkuu mmoja tu kwa sasa na anaitwa Evodius Mtawala. Simba haijawahi kuwa na makatibu wakuu wawili kwa wakati mmoja.
CHAMPIONI linafahamu ukweli huu lakini kwa sababu inazozijua lenyewe, imeamua kuandika habari hiyo na kuweka kichwa cha habari cha namna hiyo pasipo kujali athari zake kwa wanachama wa Simba, Katibu Mkuu aliyepo madarakani kwa sasa na weledi wa fani ya uandishi wa habari
Kilichoandikwa kwenye habari hiyo ya CHAMPIONI ni maoni binafsi ya mwanachama wa Simba na kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake kuhusiana na jambo lolote ali mradi halivunji sheria za nchi.
Simba SC inarudia wito wake wa kuvitaka vyombo kubaki kwenye misingi ya kitaaluma na kuacha kuandika habari zilizotiwa chumvi na kuleta mitafuruku isiyo na sababu yoyote.

Kikosi
Simba inaendelea vizuri na mazoezi visiwani Zanzibar kujiandaa na mechi dhidi ya Azam itakayopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi hii.
Hata hivyo, mchezaji Salim Kinje ameruhusiwa kuondoka kambini Zanzibar leo kutokana na kupata msiba wa baba yake mkubwa uliotokea Dar jana.
Uongozi, kwa namna ya kipekee kabisa, unatoa salamu za pole kwa familia ya Kinje kutokana na msiba huu.

Boniface Wambura
Kwa niaba yangu binafsi na klabu ya Simba, napenda kumpongeza Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, kwa kuteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa miongoni mwa wasimamizi wa shirikisho hilo katika michuano ya Wanawake itakayofanyika nchini Guinea ya Ikweta (Equatorial Guinea).
Wambura ndiye Mtanzania pekee aliyeteuliwa na CAF kutumika kwenye michuano hiyo na jambo hilo ni la faraja kwa tasnia ya habari nchini ambako Wambura ametokea.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC

No comments:

Post a Comment