Friday, October 5, 2012

NGASSA AANZA 'KUNUKA' SIMBA, ADAIWA KUCHEZA KINAZI JUZI, KAZIMOTO, BOBAN NAO NDANI, KAPOMBE AZAWADIWA MAMILIONI

Mrisho Ngassa


MRISHO Khalfan Ngassa, kiungo mpya wa Simba aliyesajiliwa baada ya ‘kufukuzwa’ Azam FC kwa kosa la kubusu jezi ya Yanga ni miongoni mwa wachezaji wanaotuhumiwa kucheza chini ya viwango vyao katika mechi ya juzi dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati beki Shomary Kapombe atazawadiwa Sh Milioni 2 ‘kwa kujituma ile mbaya’ kwenye mechi hiyo.
 
 
Simba ilifanya kikao jana kupitia mechi ya juzi na kuwatenganisha wachezaji katika makundi mawili, waliojituma na ambao hawakujituma kabisa na huko kiungo iliyemsajiki kwa mkopo kutoka Azam, Ngassa ndiye kinara.
 
 
Katika kundi la Ngassa wamo pia Haruna Moshi ‘Boban’, Mwinyi Kazimoto na Daniel Akuffo, wakati upande wa waliopiga ‘mzigo wa uhakika’, mbali na Kapombe, wengine ni Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Paul Ngalema, Juma Nyosso, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Felix Sunzu na Edward Christopher, ambao pia watazawadiwa.
 
 
Chanzo chetu kutoka Simba kimesema kwamba hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wachezaji wote ambao hawakujituma kwenye mechi hiyo, lakini si kusimamishwa wala kufukuzwa, bali kukatwa mishahara. 
 
 
“Kocha amekataa adhabu ya kufukuza mchezaji, watakatwa mishahara, ila sijui uongozi wenyewe utaenda mbali kiasi gani,”kilisema chanzo hicho.
 
 
Aidha, beki Amir Maftah na mshambuliaji Emmanuel Okwi pia nao wanaingia kwenye orodha ya wachezaji ambao hawakuwa na nia nzuri na mechi hiyo kutokana na kupewa kadi nyekundu zilizowafanya waikose mechi hiyo. “
 
Hawa wote walikuwa wana uwezo wa kuepuka zile kadi, lakini haikuwa hivyo, sasa nao uongozi unalifanyia kazi suala lao, huenda nao wakakumbwa na adhabu ya kukatwa mishahara,”kilisema chanzo hicho.
 
 
Kikao kingine kinatarajiwa kufanyika leo baina ya benchi la Ufundi na Kamati ya Ufundi na baada ya hapo hatua rasmi dhidi ya wachezaji hao zitajulikana.
 
 
Simba itafanya mazoezi leo kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam kuanzia saa 10:30 na baada ya hapo wachezaji wataingia kambini kwa ajili ya mechi ya Jumapili dhidi ya JKT Oljoro, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
 
Simba juzi ilishindwa kuendeleza ubabe wake kwa Yanga, baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wapinzani wao hao wa jadi, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuanzia saa 1:02 usiku.
 
 
Yanga ambao walimaliza mechi hiyo wakiwa pungufu baada ya Simon Msuva kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu Juma Nyosso, ndio waliohaha kusawazisha bao, baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema la kiungo Amri Kiemba.  
 
 
Hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba dakika ya pili.
 
 
Simba walicheza vizuri kipindi chote cha kwanza wakigongeana pasi za uhakika na kuwazidi kasi uwanjani wapinzani wao, wakati Yanga pamoja na kuzinduka baada ya kufungwa bao, lakini makosa yalikuwa mengi.
 
 
Pasi zao zilikuwa nyingi hazifiki, walikuwa wanapokonyeka mipira kirahisi, wanazidiwa nguvu na wapinzani wao katika kugombea mipira na hata mashambulizi yao hayakuwa ya mpangilio, zaidi ya kuonekana kubahatisha zaidi.
Katika kubahatisha huko, Mbuyu Twite alifumua shuti zuri dakika ya 38 kutoka wingi ya kulia, ambalo lilitoka nje sentimita chache.    
 
 
Kabla hata ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika, kocha Mholanzi Ernie Brandts alimtoa Hamisi Kiiza na kumuingiza Frank Domayo ili kuimarisha safu ya kiungo, ambayo ilionekana kuzidiwa na Simba inayofundishwa na Mserbia, Milovan Cirkovick.
 
 
Kipindi cha pili, Yanga walianza na mabadiliko, kocha Ernie Brandts akimtoa kiungo Nizar Khalfan na kumuingiza mshambuliaji Didier Kavumbangu, ambaye alikwenda kuongeza nguvu ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Angalau, kipindi cha pili Yanga walionekana kucheza vizuri na kupeleka mashambulizi yenye uhai langoni mwa Simba, ingawa safu imara ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi ilikuwa kikwazo.
 
 
Katika dakika ya 63, beki Paul Ngalema aliunawa mpira katika harakati za kuokoa na refa Mathew Akrama akaamuru penalti, ambayo ilikwamisha kimiani kiufundi na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
 
 
Katika dakika ya 77 Mathew Amkrama alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja Simon Msuva, baada ya kumkita Juma Nyosso, aliyemkanyaga ‘kwa bahati mbaya’. Msuva alichezewa rafu na Nyosso na tayari refa alikwishapuliza filimbi na kumpa kadi ya njano beki huyo wa Simba, lakini kiungo huyo wa Yanga akaponzwa na hasira za kitoto.
 
 
Pamoja na Yanga kubaki pungufu, waliendelea kucheza vema na mashambulizi yalikuwa ya pande zote mbili. Refa Akrama alishindwa kuumudu mchezo na maamuzi yake mengi yalikuwa chungu kwa Yanga, mfano Haruna Moshi ‘Boban’ alipomchezea rafu mbaya beki Kevin Yondan hadi akashindwa kuendelea na mchezo, na nafasi yake ikachukuliwa na Juma Abdul alimpoza kwa kadi ya njano.
Hakumchukulia hatua yoyote kipa Juma Kaseja aliyeonekana kupoteza muda tangu mwanzo, na alimpa onyo tu zaidi ya mara tatu.
 
 
Alipongia Abdul alikwenda kucheza beki ya kulia na Mbuyu Twite akahamia katikati kucheza na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
 
 
Baada ya mchezo huo, kocha wa Simba, Milovan alisema kwamba ulikuwa mchezo mzuri na Yanga walicheza vizuri, lakini timu yake ilicheza vizuri na anajivunia. Alisema Yanga imeimarika tofauti na ilivyokuwa awali na kwamba hizo ni dalili Ligi Kuu msimu huu itakuwa ngumu.
 
 
Kwa upande wake, kocha wa Yanga, mwanzoni hawakucheza vizuri, lakini baadaye walitulia na kucheza vizuri. “Hii ni mechi ya kweli ya upinzani, unaweza kuona rafu na kadi nyingi,”alisema Brandts.

No comments:

Post a Comment