Thursday, October 4, 2012

BOBAN AOMBA RADHI KWA RAFU YA YONDAN

Ilikuwa bahati mbaya, kijana ameomba radhi


KIUNGO wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ amewaomba radhi wapenzi wa soka Tanzania kwa kitendo chake cha kumchezea rafu mbaya mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kevin Yonda jana. 
 
Akizungumza  leo, Boban alisema kwamba wengi wanaweza kudhani alikusudia, lakini ukweli hadi anafika kwa Yondan hakuwa na dhamira ile. 
 
“Nia yangu ilikuwa kuukita mpira, lakini Yondan naye fundi, akautuliza ukahama, na mimi wakati huo nishauinua mguu wangu ndio unatua sasa, ukatua kwenye mguu wake.
 
 
Binafsi iliniumiza sana na kama utaona kuanzia pale sikucheza vizuri kabisa, sikuwa na raha kabisa. 
 
 
Yondan ni rafiki yangu sana, nimempokea Simba, nimeondoka nimemuacha, nimerudi, amenipokea, tumeishi vizuri, kwa kweli inaniumiza sana,”alisema Boban.
Aidha, Boban alisema kwamba atakwenda kumjulia hali Yondan na kumuomba msamaha. “Nawaomba msamaha zaidi mashabiki wa Yanga, mimi ni binadamu, wanisamahe,”alisema Boban.    
 
 
Yondan atakuwa nje kwa wiki mbili, kutokana na kuumizwa na kiungo huyo wa Simba, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
 
Daktari wa Yanga, Sufiani Juma amesema kwamba beki huyo tegemeo wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, tangu jana alikuwa anasikia maumivu makali na baada ya kufanyiwa vipimo katika Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili (MOI), imeelezwa anatakiwa kupumzika wiki mbili.
 
 
Lakini Yondan pia anaweza kukaa nje ya Uwanja kwa zaidi ya muda, huo kwani majibu hayo yanatokana na uchunguzi wa awali.
 
 
Yondan aliumizwa jana wakati Yanga ikitoka nyuma na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wapinzani wao wa jadi, Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuanzia saa 1:02 usiku.
 
 
Yanga ambao walimaliza mechi hiyo wakiwa pungufu baada ya Simon Msuva kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu Juma Nyosso, ndio waliohaha kusawazisha bao, baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema la kiungo Amri Kiemba.  
 
 
Hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba dakika ya pili, wakati Yanga ilisawazisha dakika ya 63, baada ya beki Paul Ngalema kuunawa mpira katika harakati za kuokoa na refa Mathew Akrama akaamuru penalti, ambayo ilikwamisha kimiani kiufundi na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
 
 
Katika dakika ya 77 Mathew Amkrama alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja Simon Msuva, baada ya kumkita Juma Nyosso, aliyemkanyaga ‘kwa bahati mbaya’. Msuva alichezewa rafu na Nyosso na tayari refa alikwishapuliza filimbi na kumpa kadi ya njano beki huyo wa Simba, lakini kiungo huyo wa Yanga akaponzwa na hasira za kitoto.

SIMBA, YANGA YAINGIZA MILIONI 400 KASORO KIDOGO, KLABU ZAPEWA KARIBU NUSU YA MAPATO YOTE


Juma Kaseja akidaka katika mechi ya jana

MECHI ya watani wa jadi Yanga na Simba la Ligi Kuu ya Vodacom lililochezwa jana (Oktoba 3 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1 limeingiza sh. 390,568,000.
 
 
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura Mgoyo amesema mida hii kwamba, watazamaji 50,455 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa usiku kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 93,345,549.15 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 59,578,169.49.
 
 
Amesema mgawo mwingine wa mapato hayo ni posho ya msimamizi wa kituo sh. 240,000, kamishna wa mechi sh. 250,000, waamuzi sh. 591,000, mwamuzi wa akiba (reserve referee) sh. 70,000, usafi na ulinzi wa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (stadium technical support) sh. 2,000,000.
 
 
Amesema umeme sh. 750,000, maandalizi ya uwanja (pitch preparation) sh. 400,000, ulinzi wa mechi sh. 5,860,000 wakati tiketi ni sh. 7,327,000. Gharama za mchezo sh. 31,115,183.05, uwanja sh. 31,115,183.05, Kamati ya Ligi sh. 31,115,183.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 18,669,109.83 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 12,446,073.22.
 
 
 
Wakati huo huo, Wambura amesema mechi ya ligi hiyo kati ya African Lyon na Toto Africans iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex na kushuhudiwa na washabiki tisa kwa kiingilio cha sh. 3,000 imeingiza sh. 27,000.
 
 
Amesema mgawo wa mechi hiyo ulikuwa VAT sh. 4,118.6 wakati kila timu ilipata sh. 6,864.3. Uwanja sh. 2,288.1, gharama za mchezo sh. 2,288.1, Kamati ya Ligi sh. 2,288.1, FDF sh. 1,372.8 na DRFA sh. 915.2

No comments:

Post a Comment