Tuesday, October 2, 2012

KUELEKEA PAMBANO LA WATANI; MAMBO YALIVYOKUWA MEI 6, 2012 NA VIPIGO VINGINE VYA MBWA MWIZI ALIVYOPEWA YANGA

Okwi alikuwa mwiba kwa Yanga Mei 6


SIMBA na Yanga zinamenyana kesho katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambao utarushwa moja kwa moja na Televisheni ya Super Sport ya Afrika Kusini kuanzia saa 11:00 jioni. Kabla ya mchezo wa leo, timu hizo zilimenyana Mei 6, mwaka huu katika mchezo wa kufunga msimu, je unakumbuka mambo yalikuwaje siku hiyo? Bin Zubeiry anakukumbusha…
Kikosi cha Simba msimu uliopita kilichoipiga yanga bao 5-0..kutoka kushoto waliosimama ni felix sunzu,victor costa nyumba,,boban,,mafisango,,santo,,,na walioinama toka kushoto,,nyoso,,machaku,,kaseja,,cholo,maftah,na okwii
Mambo yalivyokuwa Mei 6, Taifa hadi 5-0...
ILIKUWA ni Mei 6, mwaka 2012 wakati Wekundu wa Msimbazi, Simba SC walipokabidhiwa Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania kwa shangwe nzito, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kuwabwaga wapinzani wao wa jadi, Yanga mabao 5-0.
Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi mawili, Juma Kaseja, Felix Sunzu na Patrick Mutesa Mafisango.
Hicho kilikuwa kipigo cha pili kikali kihistoria Simba wanaifunga Yanga, baada ya zile 6-0 za mwaka 1977.
Ilikuwa ni hoi hoi, nderemo na vifijo kuanzia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hadi kona mbalimbali za Jiji, rangi nyekundu na nyeupe zikiwa zimetawala na shangwe za Simba.
Hadi mapumziko, Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi dakika ya pili tu ya mchezo huo.
Okwi alimtungua kipa Mghana, Yaw Berko baada ya kutumia mwanya wa kuzubaa kwa mabeki wa Yanga mwanzoni mwa mchezo huo.
Katika kipindi hicho, Okwi alikuwa akimpita kwa urahisi beki mkongwe wa Yanga, Nsajigwa Shadrack Joel Mwandemele ambaye aliishia kumkwatua mara kwa mara, jambo ambalo lilimponza kwenda chumba cha kupumzikia akiwa ana kadi moja ya njano aliyopewa dakika ya 39.
Pamoja na kufungwa bao hilo, Yanga waliendelea kucheza kwa utulivu, wakigongeana pasi vizuri na kutengeneza nafasi kadhaa, ingawa kikwazo kilikuwa Tanzania One, Juma kaseja.
Nafasi pekee nzuri katika kipindi hicho na ambayo Yanga wataijutia waliipata dakika ya 35, baada ya Mwanasoka Bora wa Uganda, Hamisi Kiiza kuwatoka vizuri mabeki wa Simba, lakini akiwa amebaki yeye na kipa, hesabu zake ziliendana na Kaseja.
Kiiza aliupelekea mpira upande wa kushoto wa kipa huyo bora Tanzania, ambaye naye akachupa upande huo huo na kuokoa.
Kipindi cha pili, Yanga walianza kwa mabadiliko, wakimtoa kipa Yaw Berko na kumuingiza Said Mohamed Kasarama, wakati Simba walimpumzisha Mwinyi Kazimoto na nafasi yake kuchukuliwa na Jonas Mkude.
Simba waliingia tena kwa kasi na kufanikiwa kupata mabao matatu ya haraka haraka, mawili yakipitia kwa Nsajigwa.
Bao la pili la Simba lilitokana na penalti, baada ya Nsajigwa Shadrack kumkwatua Okwi kwenye eneo la hatari na Felix Sunzu akaenda kufunga kwa penalti dakika ya 56.
Okwi alifunga bao la tatu dakika ya 62, baada ya kumtoka Nsajigwa Fusso na kumchambua kipa Said Mohamed Kasarama.
Baada ya bao hilo, kocha Fred Felix Minziro alipumzishwa Nsajigwa na kumuingiza Godfrey Taita Magina. 
Dakika ya 67 Uhuru Suleiman aliangushwa na Taita kwenye eneo la hatari na Juma Kaseja akaenda kufunga bao la nne kwa penalti. Patrick Mafisango (sasa marehemu) alifunga bao la tano kwa penalti pia dakika ya 72.
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango/Obadia Mungusa, Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto/Jonas Mkude, Felix Sunzu/Edward Christopher, Haruna Moshi ‘Boban’ na Emmanuel Okwi.
Yanga: Yaw Berko/Said Mohamed, Nsajigwa Shadrack/Godfrey Taita, Oscar Joshua, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’, Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Davies Mwape/Kenneth Asamoah, Rashid Gumbo na Hamisi Kiiza.
Naam, hivi ndivyo mambo yalivyokuwa Mei 6, 2012 na baada ya hapo Yanga wakafanya mabadiliko makubwa ya uongozi, wakimtoa Mwenyekiti wao wa wakati huo, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga na kuweka safu mpya ya uongozi, chini ya Mwenyekiti Yussuf Manji.
Je, kesho tutarajie nini Uwanja wa Taifa, miamba hiyo ikikutana tena? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
Okwi na Fusso siku hiyo...palikuwa patamu shandrack nsajigwa alikuwaga njia mpaka sasa hawamwamini katika kikosi kile pale aliposababisha bao za penalti
VIPIGO VINGINE VYA ‘MBWA MWIZI’ SIMBA WALIVYOICHAPA YANGA:
LIGI KUU BARA:
JULAI 19, 1977
Simba v Yanga
6-0
WAFUNGAJI:
Abdallah Kibadeni dk. 10, 42 na 89, Jumanne Hassan 'Masimenti' dk. 60 na 73, Selemani Sanga alijifunga dk. 20.
JULAI 2, 1994
Simba v Yanga
4-1
WAFUNGAJI:
Simba: George Masatu, Athumani China, Madaraka Selemani, Dua Saidi Yanga; Constantine Kimanda.
MACHI 31, 2002.
Simba Vs Yanga 4-1 (Kombe la Tusker)
WAFUNGAJI:
SIMBA: Mark Sirengo dk. 3 na 76, Madaraka Selemani dk. 32 na Emanuel Gabriel dk. 83.
YANGA: Sekilojo Chambua dk 16.
(Mechi hii ya fainali iliyohudhuriwa na rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, chupuchupu ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa. Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga. Mwamuzi wa mchezo huo, Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo. Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania, FAT).
MEI 6, 2012
Samba 5-0 Yanga SC
WAFUNGAJI:
Emmanuel Okwi (dk 2 na 62), Felix Sunzu (penalti 56), Juma Kaseja (penalti dk 67) na Patrick Mafisango (penalti dk 72)

No comments:

Post a Comment