Sunday, September 30, 2012
VODACOM BADO IPO IPO SANA LIGI KUU BARA
![]() |
Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa |
BAADA ya kikao cha pamoja cha majadiliano kati ya Mdhamini mkuu wa Ligi Kuu Vodacom
Tanzania Bara, Kamati ya ligi, TFF na klabu zinazoshiriki ligi hiyo, mashabiki na wapenzi wa soka nchini
wameondolewa hofu juu ya udhamini wa ligi inayoendelea hivi sasa.
Mdhamini mkuu
wa ligi hiyo Vodacom Tanzania, imekubali kuendelea kuunga mkono ligi hiyo na
kuwaomba mashabiki wa soka kutegemea msimu mzuri wa ligi mwaka huu.
Kwa mujibu wa
Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa,
amesema kuwa mvutano ambao umekuwepo baina ya baadhi ya Vilabu vya soka na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na wadhamini sasa yamepatiwa
ufumbuzi.
“Kulikuwa na
sinto fahamu kati ya Klabu za ligi kuu TFF na sisi kama wadhamini, tulikaa
kikao siku ya ijumaa na wadau wote wa ligi na sasa mambo yote yamewekwa katika
msitari,” alisema Kelvin na kuongeza kuwa “ Tumedhamiria kuendelea kuiunga
mkono Ligi kuu ya Vodacom hatukuwa na matatizo yoyote katika kusaini mkataba na
kamati ya ligi ni ufafanuzi tu ndio ulihitajika ili kuwekana sawa,” alisema Twissa.
Kuhusiana na
kutolewa kwa fedha za udhamini na uendeshaji wa ligi na udhamini wa kampuni
pinzania twissa alisema Vodacom haizuii klabu za ligi kudhaminiwa na kampuni
nyingine yoyote tofauti na zile zenye msingi wa kiushindani katika biashara na
kampuni hiyo.
“Kufuatia
kikao hicho na kuwa katika msitari mmoja tumekwisha toa fedha na vifaa kwa TFF
na vilabu ili ligi iweze kwenda kama ilivyo takiwa,Tukiwa kama wadau katika
kuunga mkono maendeleo ya soka nchini, tumeruhusu kampuni nyingine ambazo
hazina upinzani wa kibiashara na sisi ili kuondoa muingiliano wa kimaslahi,”
alisema.
“TFF
inadhamana ya kusimamia sheria na masharti kuhusu ligi. Hatuna matatizo yoyote
ya kiutendaji na TFF wala klabu yoyote” alihitimisha Twissa.
Ligi kuu ya Vodacom ilianza rasmi
tarehe 15 mwezi septemba, na tutashuhudia
michezo 182 kwa kushirikisha timu 14 zinazoshiriki katika ligi hiyo, zikiwemo
Yanga Afrika, Kagera sugar, na Simba ambaye ndie bingwa mtetezi wa ligi kuu ya
Vodacom.
Kampuni ya Vodacom
imekuwa mdhamini wa ligi kuu kwa miaka mitano sasa, na imesaini mkataba mpya wa
udhamini wa ligi hiyo kwa miaka mitatu na shirikisho la mpira wa miguu TFF,
mkataba utakao shuhudia shirikisho hilo likipokea udhamini wa kila msimu kwa
miaka mitatu mfululizo.
SIMBA WAKIPIGA NA ZANZIBAR ALL STARS LEO USIKU AMAAN
SIMBA SC inatarajiwa
kushuka dimbani kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar kuanzia saa 2:00 leo kumenyana
na All Stars ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki, kujiandaa na mpambano dhidi
ya watani wao wa jadi, Yanga Jumatano, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba imerejea
leo Zanzibar, baada ya jana kuendeleza wimbi lake la ushindi katika Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, kwa kuichapa Prisons ya Mbeya iliyorejea Ligi Kuu msimu
huu mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mabao ya
Simba yalitiwa kimiani na Felix Mumba Sunzu na Mrisho Ngassa, ambaye hilo ni
bao lake la kwanza katika Ligi Kuu ndani ya mechi nne na la pili jumla tangu
ajiunge na timu hiyo katika mechi saba alizocheza, wakati la Prisons lilifungwa
na Elias Maguri.
Kwa ushindi
huo, Simba imefikisha pointi 12 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, ikiizidi Azam
FC pointi mbili katika nafasi ya pili, ingawa timu zote zimecheza mechi sawa,
nne.
Hadi
mapumziko, timu hizo zilikuwa zikwishafungana bao 1-1, Prisons wakitangulia
kupata bao dakika ya sita baada ya Maguri kuwatoka mabeki wa Simba kupiga shuti
lililomgonga Shomary Kapombe na mpira kupoteza mwelekeo na kumchanganya kipa na
Nahodha wa Simba, Juma Kaseja na kutinga nyavuni.
Baada ya bao
hilo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, ingawa Prisons waliendelea
kuwa wagumu, hadi walipojisahau kidogo sekunde za mwishoni za kipindi cha
kwanza na Felix Sunzu akatumia pasi ya Amiri Maftah kusawazisha dakika ya 45.
Kipindi cha
pili, Simba walirudi na moto na kuanza moja kwa moja kulishambulia mfululizo
lango la Prisons na dakika ya 55 Ngassa akafunga kwa shuti dhaifu, ambalo kipa wa
Prisons, David Abdallah alidaka lakini mpira ukamtoka na kuingia nyavuni.
Mechi hiyo
ilichezeshwa na refa, Paul Soleji kutoka Mwanza, aliyesaidiwa na Jesse Erasmo,
mshika kibendera namba moja, Mwarabu Mumba mshika kibendera namba mbili, wote
kutoka Morogoro, wakati refa wa Akiba alikuwa Israel Nkongo wa Dar es Salaam.
Dakika ya 87
Amir Maftah alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Khalid Fupi wa Prisons,
hivyo ataukosa mchezo ujao dhidi ya Yanga Jumatano na hiyo ni nafasi kwa
chipukizi Paul Ngalema.
Hiyo inakuwa
kadi ya pili nyekundu kwa Simba ndani ya mechi nne, awali katika mechi ya pili
dhidi ya JKT Ruvu, Emmanuel Okwi alilimwa kadi ya aina hiyo kwa kumpiga kiwiko
Kessy Mapande na akafungiwa mechi tatu.
Kikosi cha
Simba jana kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomari
Kapombe, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba/Salim Kinje, Ramadhan Chombo/Jonas
Mkude, Christopher Edward/Daniel Akuffo, Felix Sunzu na mrisho Ngassa.
Prisons: 18.David Abdallah, 03.Aziz Sibo, 05.Laurian Mpalile, 16.Lugano Mwangama (Nahodha), 15.David Mwantika, 13.Khalid Fupi, 07.Misango Magai, 12.Fred Chudu/22.Julius Kwaga, 14.Elias Maguri, 17.Peter Michael/Sino Augustino na 19.John Matei/11.Hamisi Ally.
No comments:
Post a Comment