Saturday, February 2, 2013

KMKM YAANZA VEMA LIGI KUU ZBAR



KMKM imeanza vyema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Zanzibar, maarufu kama Zanzibar Grand Malt Premier League, baada ya kuichapa Mafunzo mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung, Kisiwani Unguja jana.
KMKM ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wao tegemeo Maulid Ibrahim katika dakika ya 35 ya kipindi cha kwanza, mpaka mapumziko matokeo yalikuwa yanasomeka 1-0.
Kipindi cha pili katika mchezo huo kiliingia dosari baada ya mchezaji wa KMKM Faki Mwalim kutolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia mchezo mbaya.
Mafunzo walifanikiwa kusawazisha katika dakika ya 79 kupitia kwa Ame Khamis, hata hivyo bao hilo halikudumu kwani licha ya KMKM kucheza pungufu mchezaji mmoja walifanikiwa kupata bao la ushindi katika dakika ya 82 kupitia kwa Jaku Joma.
Kwa matokeo hayo KMKM wanaendelea kuongoza msimamo wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 26 wakifuatiwa na Mafunzo yenye pointi 22.
Katika mchezo mwingine, uliofanyika kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Super Falcon wamefanikiwa kuanza vyema mzunguko wa pili baada ya leo kuchomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chipukizi ya Chake Chake.
Bao pekee la ushindi kwa Super Falcon lilifungwa katika dakika na Omar Mohammed katika dakika ya 69.
Ligi hiyo inatarajia kuendelea tena kesho katika viwanja viwili tofauti katika visiwa vya Unguja na Pemba. Kisiwani Pemba katika Uwanja wa Gombani kutakuwa na pambano kati ya Duma timu inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Uchumi Kisiwani Pemba, ikionyeshana kazi na Jamhuri ambao tarehe 16 ya mwezi huu watakuwa na mechi ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika watakapoikaribisha St. George kutoka Ethiopia kabla ya kurejeana wiki mbili baadae, itakumbukwa kuwa Jamhuri ambao ni washindi wa pili wa ligi iliyopita walitakiwa kuiwakilisha Zanzibar katika kombe la Shirikisho lakini kutokana na Mabingwa wa Soka Zanzibar kuamua kujitoa katika michuanop hiyo kutokana na ukata Jamhuri wamechukua nafasi hiyo huku Zanzibar ambao ni mwanachama mshiriki wa CAF wakiwa hawana uwakilishi katika michuano ya kombe la Shirikisho inayoandaliwa na CAF.
Kwa upande wa Kisiwa cha Unguja hapo kesho kutakuwa na mchezo mmoja katika Uwanja wa Amaan, ukiwakutanisha Bandari na Malindi.

No comments:

Post a Comment