Wednesday, January 23, 2013

YANGA INATARAJIA KUWATWANGA TENA VIBONDE WA LIGI KUU SOUTH AFRICA BLACK LEOPARD CMM KIRUMBA MWANZA


Yanga SC
YANGA SC inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza leo kumenyana na Black Leopard ya Afrika Kusini, huo ukiwa mchezo wa pili kuzikutanisha timu hizo ndani ya siku nne.
Awalil, timu hizo zilimenyana Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Yanga ikashinda mabao 3-2.
Huo utakuwa mchezo wa mwisho wa kujipima nguvu kwa Yanga, kabla ya kuingia mzunguko wa pili wa Ligi Kuu hya Vodacom Tanzania Bara unaoanza mwishoni mwa wiki.
Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, katika kujiandaa na mzunguko huo wa pili wa Ligi Kuu, waliweka kambi ya wiki mbili Jijini Antalya, Uturuki kuanzia Desemba 30 mwaka jana hadi Januari 12 mwaka huu.
Katika kambi hiyo, pamoja na kufanya mazoezi ya nguvu ya ufukweni, uwanjani na gym, Yanga ilipata mechi tatu za kujipima nguvu dhidi ya Ariminia Bielefed ya Daraja la Nne Ujerumani waliyotoka nayo sare ya 1-1, kabla ya kufungwa 2-1 na Denizlispor FC ya Daraja la Kwanza Uturuki na 2-0 na Emmen FC ya Daraja la Kwanza Uholanzi.
Yanga ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 29, baada ya kucheza mechi 13, ikifuatiwa na Azam iliyomaliza na pointi zake 24 na mabingwa watetezi, Simba SC waliomaliza na pointi 23.  
Katika mchezo wa kwanza na Leopard Dar es Salaam, hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na mshambuliaji wake aliyefufua makali, Jerry John Tegete dakika ya 33.
Tegete, alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti, baada ya kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Niyonzima kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki Nkosiyaba Xakane na refa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam akatoa adhabu hiyo.
Kipindi cha pili, kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts alifanya mabadiliko, akiwatoa pacha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wenye uraia wa Rwanda, Mbuyu Twite na Kabange Twite na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na kuwaingiza Simon Msuva, Juma Abdul na kipa Said Mohamed.
Mabadiliko hayo, hayakuisaidia Yanga, kwani Leopard walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya kwanza tu tangu kuanza kipindi cha pili, lililofungwa kwa kichwa na Humphrey Khoza aliyetumia udhaifu wa mabeki wa timu hiyo ya Jangwani na kumtungua kipa Said Mohamed Kasarama.     
Baada ya kufungwa bao hilo, Yanga walicharuka na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 63, lililofungwa na Frank Domayo aliyeunganisha krosi maridadi ya Niyonzima.
Jerry Tegete aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 72 akiunganisha pasi ya beki Juma Abdul na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo waruke kwa shangwe za ‘Uturuki, Uturuki’, kuashiria hayo ni matunda ya ziara ya timu hiyo nchini Uturuki.
Beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alimuangusha kwenye eneo la hatari Humphrey Khoza dakika ya 88 na refa akawapa penalti Leopard ambayo ilikwamishwa kimiani na Rodney Romagalela na kufanya matokeo yawe 3-2.
Katika mchezo wa leo, vikosi vinatarajiwa kuwa, Yanga; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Stefano Mwasyika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Kabange Twite, Frank Domayo, Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Haruna Niyonzima.
Black Leopard; Ayunda Mtshati, Ernort Zaga, Nkosiyaba Xakane, Harry Nyirenda, Humphrey Khoza, Muganga Dyange Jean, Mongezi Bobe, Thomas Madiba, Abbas Amidu, Edgar Manake na Rodney Romagalela. 

No comments:

Post a Comment