Sunday, January 20, 2013

MSHAMBULIAJI WA ZAMANI W ATIMU YA TAIFA ALIYEING'ARISHA STARS DHIDI YA SENEGAL MWAIKIMBA AITAKATISHA AZAM NAIROBI, YAIPIGA SOFAPAKA KWAO


Shujaa wa Azam leo, Mwaikimba

BAO pekee la Gaudence Exavery Mwaikimba kwa penalti dakika ya 58, jioni hii limeipa Azam FC ushindi wa 1-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Sofapaka ya Kenya kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
Huo ni ushindi wa kwanza wa Azam katika ziara yake ya wiki moja nchini Kenya, baada ya jana kufungwa 2-1 na AFC Leopard kwenye Uwanja huo huo wa Nyayo.
Penalti hiyo, ilitolewa baada ya beki mmoja wa Sofapaka, kuunawa mpira uliopigwa na kiungo Mkenya, Humphrey Mieno.
Akiuzungumzia ushindi huo, Kocha wa Azam Muingereza Stewart Hall alisema hii inamaanisha timu yake sasa imeimarika kiasi cha kutosha na ndiyo maana inashinda mechi hata nje ya nchi.
Pamoja na kufungwa jana na Leopard, Azam watajilaumu wenyewe, kwani walipoteza penalti mbili kupitia kwa Joackins Atudo na Khamis Mcha ‘Vialli’.
Mabao ya Leopard katika mchezo wa jana, yalifungwa na Paul Were na Mike Barasa, wakati la Azam lilifungwa na Sammih Hajji Nuhu kwa penalti.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Salum, Himid Mao/Malika Ndeule, Samir Hajji Nuhu, David Mwantika/Luckson Kakolaki, Joackins Atudo, Kipre Balou/Abdulhalim Humud, Seif Abdallah, Salum Abubakar, Brian Umony/Jabir Aziz, Humphrey Mieno/Gaudence Mwaikimba na Khamis Mcha/Uhuru Suleiman.
Azam itashuka dimbani Jumanne, kucheza mechi ya mwisho na timu ya Benki ya Biashara ya Kenya, KCB kwenye Uwanja wa City na Jumatano watapanda basi lao kuvuka boda la Namanga kurejea nyumbani Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment