Thursday, January 17, 2013

MKALI WA MABAO WA AZAM BOCCO, NA KIPRE TCHETCHE WAACHWA SAFARI YA KENYA AZAM


Azam FC
WASHAMBULIAJI wa Azam FC ya Dar es Salaam, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ na Kipre Herman Tchetche, wameachwa katika safari ya klabu yao hiyo nchini Kenya kutokana na kuwa bado majeruhi.
Azam imeondoka leo Alfajiri kwenda Kenya kwa ziara ya wiki moja ya kucheza mechi za kujipima nguvu kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Katibu wa Azam FC, Nassor Idrisa amesema  kwamba wachezaji wote wa klabu wameondoka na timu kasoro wawili hao ambao wataendelea kusikilizia hali zao na watajiunga na timu ikirejea safari hiyo.
Ikiwa Nairobi katika ziara hiyo, mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi watacheza mechi tatu za kujipima nguvu dhidi ya timu za Sofapaka, AFC Leopards na Gor Mahia kabla ya kurejea nchini Januari 23.
Nassor alisema ziara hiyo ni maalum kwa ajili ya kuiweka sawa timu yao kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Nassor amesema anaamini timu za Kenya ni nzuri na zitawapa changamoto nzuri kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na kuingia kwenye Kombe la Shirikisho.
“Tumekuwa katika programu ndefu ya maandalizi tangu Desemba, tukianzia Kongo (DRC) ambako tulicheza mashindano na kuchukua Kombe, tumetoka tumeingia kwenye Kombe la Mapinduzi tumeshiriki na kuchukua Kombe, na sasa tunakwenda Kenya,”alisema Nassor.
Jumamosi iliyopita Azam ilitetea Kombe lake la Mapinduzi, baada ya kuichapa mabao 2-1 Tusker ya Kenya katika fainali kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Awali ya hapo, Desemba mwaka jana Azam ilitwaa Kombe la Hisani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)

No comments:

Post a Comment