Wakati Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, akitamka
kuwa Mkutano wa Wanachama uliotishwa na Kundi linalodaiwa kuongozwa na
Mohamed Wandi si halali, zipo taarifa kuwa Kocha mpya wa Klabu hiyo,
Patrick Liewing, kutoka Ufaransa atatuaNchini leo.
Akizungumzia Mkutano huo ulioitishwa na
Kundi la Mohamed Wandi ambalo limeripotiwa kukusanya Saini za Wanachama
698 ili kufanya Mkutano wa Wanachama Jumapili hii kwenye Hoteli ya
Traventine Jijini Dar es Salaam, Rage amesema uchunguzi wa Watu hao 698
umebaini kuwa 490 kati yao si Wanachama hai kwa vile hawajalipa Ada zao
za Uanachama na wengine kati yao ni Marehemu.
Akithibitisha kupokea Barua ya kuitishwa
Mkutano huo wa Dharura wa Wanachama, Rage amesema Kikatiba mwenye
mamlaka ya kuitisha Mkutano wa Dharura wa Wanachama ni Mwenyekiti au
Wanachama hai 600.
Kutokana na hitilafu hizo za Kisheria, Rage amesema Uongozi wake hautautambua Mkutano huo.
Pia, Rage amedai Kundi la Viongozi wa zamani ndio wanaotaka kuitisha Mkutano huo kinyume cha Katiba yao.
Hata hivyo, Mohamed Wandi amekaririwa
akitamka kuwa Mkutano huo hauna nia mbaya ila tu ni kuchambua mwendo
mbovu wa Simba katika mzunguko wa Kwanza wa Ligi Kuu Vodacom ambao
walianza vizuri mno lakini wakamaliza vibaya na kutupwa nafasi ya 3 huku
juu yao wapo Azam FC na vinara ni Mahasimu wao wakubwa, Yanga.
Wakati huo huo, Ismail Aden Rage,
amethibitisha ujio wa Kocha wao mpya, Patrick Liewing, kutoka Ufaransa
ambae atatua Nchini leo.
Rage amesema Kocha huyo, ambae aliwahi
kufundisha Timu za Vijana za Klabu maarufu huko France, Paris Saint
Germain, atakuwa Kocha Mkuu na pia atapewa jukumu la kuendeleza vipaji
vya Vijana.
Rage amesema: “Simba ndio Timu pekee
Nchini yenye mfumo wa kuendeleza Vijana na zipo timu za Vijana chini ya
Miaka 14, 16 17 na 20! Ujio wa Liewing utatusaidia sana kwa sababu ana
uzoefu wa kukuza vipaji!”
Kocha huyo mpya kesho anatarajiwa kukutana na Wachezaji wote kwenye Kambi yao ya Mazoezi huko TCC Chang’ombe, Dar es Salaam.
Liewing, ambae anambadili Kocha kutoka
Serbia Milovan Cirkovic, aliwahi kuwa Kocha wa Asec Mimosa ya Ivory
Coast kati ya Mwaka 2004 na 2009 na kuisaidia kutwaa Makombe kadhaa
Nchini humo pamoja na kuifikisha Nusu Fainali ya CAF CHAMPIONZ LIGI
Mwaka 2009.
Mwaka 2006, Kocha Liewing pamoja na Kocha wa Al Ahly ya Misri waliteuliwa kuwa Makocha Bora Afrika.
No comments:
Post a Comment