Sunday, January 13, 2013

UKATA WA MASHABIKI MAPINDUZI WAONEKANA BAADA YA KUPATA SHILINGI MIL.41 TU KWA MECHI 15



JUMLA ya Sh. Milioni 41.3 zimepatikana kutokana na viingilio vya mechi za Kombe la Mapinduzi, michuano iliyomalizika visiwani hapa jana kwa Azam FC kuibuka bingwa kwa mara ya pili mfululizo.
Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Aman Ibrahim Makungu alisema jana kwamba, hadi jana wamepata kiasi hicho tu cha fedha kutokana na viingilio.
Aidha, Makungu amesema wadhamini wa michuano hiyo wamechangia kiasi cha Sh. Milioni 67 na kwamba hiyo ndiyo siri ya kufanikiwa kwa mashindano ya mwaka huu ya Kombe la Mapinduzi.
Mapato hayo yanatokana na jumla ya mechi 15 za mashindano ya mwaka huu hadi fainali jana, kuanzia hatua ya makundi. Timu nane zilishiriki mashindano haya, ambazo ni Simba SC ya Dar es Salaam, Tusker FC ya Kenya, Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba zilizokuwa Kundi A, Azam FC ya Dar es Salaam, Mtibwa Sugar ya Morogoro, Coastal Union ya Tanga na Miembeni ya Unguja zilizokuwa Kundi B.
Kutoka Kundi A, Tusker walifuzu kama vinara, wakati Simba SC walifuzu kama washindi wa pili na Kundi B Azam FC walifuzu kama washindi wa kwanza na Miembeni washindi wa pili. Katika Nusu Fainali, Azam iliitoa Simba SC kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 120, wakati Tusker walitumia dakika 90 kuibanjua Miembeni 2-0.
Azam FC jana usiku walitetea Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar baada ya kuifunga Tusker FC ya Kenya mabao 2-1.
Kwa ushindi huo, Azam walizawadiwa Sh. Milioni 10, wakati washindi wa pili Tusker wamepata Sh. Milioni 5
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ramadhan Rajab Ibada ‘Kibo’ aliyesaidiwa na Mwanahija Makame Mfumo na Mgaza Kindundi, hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao.
Azam ndio walioshambulia zaidi katika kipindi hicho, lakini hawakuwa na bahati ya kufunga bao japo moja. Gaudence Mwaikimba alipewa pasi nzuri na Brian Umony dakika ya 44, lakini shuti lake kali lilidakwa na kipa Samuel Odhiambo.
Kipindi cha pili, Tusker walirudi na moto mkali na kuanza kusukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa Azam.
Hiyo iliwasaidia mabingwa hao wa Kenya kupata bao dakika ya 60, lililofungwa na Jesse Were aliyeunganisha kwa shuti kali la kimo cha mbuzi pasi ya Robert Omunok.
Hata hivyo, bao hilo halikudumu sana, kwani Azam FC walisawazisha dakika ya 72 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na beki Mkenya, Joackins Atudo baada ya beki wa Tusker, Luke Ochieng kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Katika dakika mbili za nyongeza baada ya kutimu kwa dakika 90 za mchezo huo, alijitokeza binti mwenye umri kati ya 14 na 16 na kukatiza uwanjani akitokea jukwaa la Urusi.
Refa alijaribu kumsimamisha, lakini aliendelea kukatiza Uwanja hadi nje ambako alipokewa na askari Polisi na kutolewa nje kabisa ya Uwanja. Mtangazaji wa Uwanja wa Amaan, Farouk Karim aliwatuliza mashabiki akisema binti huyo ametoroka hospitali ya vichaa, Kidongo Chekundu na tayari Polisi wamemkamata na kumrejesha huko.
Hadi dakika 90 zinamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1 na ndipo zikaongezwa dakika 30.
Gaudence Exavery Mwaikimba aliipatia Azam bao la ushindi dakika ya pili tu tangu kuanza kwa muda wa nyongeza baada ya kuwazidi nguvu na maarifa mabeki wa Tusker.
Aidha, Jesse Were mshambuliaji wa Tusker aliibuka mfungaji bora kwa mabao yake matano na kuzawadiwa Sh. 300,000, akifuatiwa na Joackins Atudo wa Azam aliyefunga mabao matatu sawa na Adeyum Saleh Ahmed wa Miembeni.
WAFUNGAJI WA MABAO:
Jesse Were                     Tusker FC     5
Joackins Atudo                Azam FC       3
Adeyum Saleh                 Miembeni      3
Gaudence Mwaikimba      Azam FC      2
Haruna Chanongo            Simba SC    2
Mfanyeje Mussa               Jamhuri        2
Michael Olunga                Tusker FC    2
MATOKEO YA MECHI ZOTE KOMBE LA MAPINDUZI 2013:
Janauri 2, 2013
Tusker 5-1 Bandari
Simba SC 2-2 Jamhuri
Januari 3, 2013
Mtibwa Sugar 1-4 Miembeni
Azam FC 0-0 Coastal Union  
Januari 4, 2013
Jamhuri 2-1 Bandari
Simba SC 1-1 Tusker FC
Januari 5, 2013
Mtibwa Sugar 1-1 Coastal Union
Miembeni 1-2 Azam
Januari 6, 2013
Tusker 1-0 Jamhuri
Simba SC 1-1 Bandari
Januari 7, 2013
Miembeni 0-0 Coastal Union
Azam FC 0-0 Mtibwa Sugar
Januari 9, 2013; NUSU FAINALI
Azam FC 2-2 Simba SC (penalti 5-4)
Januari 10, 2013; NUSU FAINALI
Tusker FC 2-0 Miembeni FC
Januari 12, 2013; FAINALI
Azam FC 2-1 Tusker FC
ORODHA YA MABINGWA KOMBE LA MAPINDUZI
2003   Mtibwa Sugar
2004   Yanga SC
2005   Yanga SC
2006   Simba SC
2007   Yanga SC
2008   Simba SC
2009   Miembeni FC
2010   Mtibwa Sugar
2011   Simba SC
2012   Azam FC
2013   Azam FC

No comments:

Post a Comment