Thursday, January 10, 2013

MNYAMA AENDA OMAN AKIKUMBUKIA ICECREAM ZA AZAM KULAMBISHWA JANA NA AZAM NA KUTINGA FAINALI MAPINDUZI


Wachezaji wa Azam wakiwa wamembeba shujaa wao wa leo Malika Ndeule
AZAM FC imeingia Fainali ya Kombe la Mapinduzi usiku huu, baada ya kuifunga Simba SC kwa penalti 5-4, kufuatia sare ya kufungana mabao 2-2 ndani ya dakika 120 usiku huu kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani hapa.
Hadi mapumziko, Azam FC walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na kiungo Mkenya, Humphrey Mieno dakika ya 10, akiunganisha kwa kichwa kona maridadi iliyochongwa na kiungo mzalendo, Ibrahim Mwaipopo.
Azam ilishambulia zaidi baada ya bao hilo, kabla ya Simba kuzinduka dakika tatu baadaye na kuanza kushambulia pia.
Mchezo huo ulisimama kwa dakika tano kuanzia ya 14 hadi 19 kutokana na umeme kukatika uwanjani hapo, hali iliyolazimisha kuwashwa kwa Jenereta.
Kipindi cha pili Simba walibadilika mno kiuchezaji na kuanza kutawala mchezo jambo ambalo liliwasaidia kupata bao la kusawazisha dakika ya 78, ambalo lilifungwa na Rashid Ismail.
Simba ilipoteza nafasi mbili za wazi za kufunga mabao ndani ya dakika 45 za kipindi cha pili na mchezo ukamalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1.
Katika dakika 30 za nyongeza, Simba walifanikiwa kupata bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 110, mfungaji Miraj Madenge.
Azam walionekana kupagawa baada ya kupigwa bao la pili na kuanza kucheza rafu za ovyo na kutoa maneno machafu kwa refa, jambo ambalo liliwaponza kupoteza wachezaji wawili ndani ya dakika mbili.
Refa Waziri Shekha alianza kumtoa nje kwa kadi nyekundu kiungo Mwaipopo dakika ya 114 na baadaye Jabir Aziz dakika ya 116.  
Wakati refa huyo akijiandaa kupuliza kipyenga cha kuhitimisha mchezo na mashabiki wa Simba wakiwa wameuteka Uwanja wa Amaan kwa shangwe zao, beki Emily Mgeta alimuangusha kwenye eneo la hatari beki Malika Ndeule na hivyo kuwa adhabu ya penalti.
Malika amebebwa juu juu
Beki Mkenya, Joackins Atudo ambaye amekuwa akipewa dhamana ya kupiga penalti kwa sasa Azam FC, alikwenda kupiga mkwaju huo na kuukwamisha nyavuni kuwapatia Watoto wa Bakhresa bao la kusawazisha.
Kutoka hapo, mchezo ulihamia kwenye mikwaju ya penalti na usiku huu bahati haikuwa yake kiungo matata chipukizi wa Simba, Haroun Athumani Chanongo, kwani pamoja na kupiga penalti nzuri iliyokuwa ya pili kwa timu yake, iligonga mwamba wa juu katikati na kudunda chini kisha kurejea uwanjani.
Wachezaji wa Simba waliofunga penalti zao leo ni Komabil Keita ya kwanza, Jonas Mkude ya tatu, Miraj Adam ya nne na Ramadhani Mkiparamoto ya tano, wakati wa Azam waliofunga ni Gaudence Mwaikimba ya kwanza, Himid Mao ya pili, Atudo ya tatu, Samir Hajji Nuhu ya nne na Malika Ndeule ya tano.
Kwa matokeo hayo sasa, Azam itamenyana na mshindi wa kesho kati ya Tusker na Miembeni katika fainali Jumamosi.
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; William Mweta, Miraj Adam, Paul Ngalema, Hassan Khatibu/Hassan Isihaka dk89, Komabil Keita, Jonas Mkude, Ramadhani Singano/Miraj Madenge dk71, Abdallah Seseme/Said Demla dk 61, Rashid Ismail, Marcel Kaheza/Ramadhan Mkipalamoto dk72 na Haroun Chanongo.
Azam FC; Mwadini Ally, Himid Mao, Samir Hajji Nuhu, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Seif Abdallah/Gaudence Mwaikimba dk69, Ibrahim Mwaipopo, Brian Umony/Malika Ndeule dk104, Humphrey Mieno/Jabir Aziz dk79 na Uhuru Suleiman.

No comments:

Post a Comment