Sunday, December 23, 2012

MABINGWA WA AFRIKA MASHARIKI NA KATI YANGA YA DAR ES SLAAM KWENDA UTURUKI


Baadhi ya wachezaji wa Yanga wataachwa hapa nyumbani wakati timu hiyo itakapokwenda Uturuki kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Bara wiki ijayo.

  Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, amesema baadhi ya wachezaji wataachwa katika safari hiyo; ambayo imekosolewa kutokana na nchi za Ulaya kuwa katika kipindi cha majira ya Baridi kali  kwa sasa.

 Kocha ndiye mwenye maamuzi ya mwisho ya kujua ni wachezaji gani ataondoka nao kwenda kwenye kambi hiyo, amesema Sanga ambaye alisisitiza kikosi cha timu hiyo kitaondoka Ijumaa licha ya nchi hiyo kuwa katika kipindi cha baridi.

Kiwango cha chini cha joto katika jiji la Ankara, Uturuki kwa siku nne kuanzia leo ni kati ya nyuzi 4-6 sentigredi, ikiwa ni baridi zaidi kwa alama 27 kulinganisha na hali ya hewa ya Dar es Salaam.

Sanga hakutaja majina wala idadi ya wachezaji watakaochwa miongoni mwa 28 waliopo sasa kwa maelezo kuwa ni jukumu la mwalimu.

 Mipango ya kuipeleka timu hiyo imekamilika na Yanga inasubiri siku ya safari tu,  na kueleza zaidi kuwa:

Kocha Ernest Brandts amekubaliana na uongozi kuipeleka timu hiyo nchini Uturuki kwa ajili ya kambi hiyo.

"Hakuna tatizo na safari hii, tulikuwa kwenye vikao kujadili jambo hili na tumeamua timu iondoke kama ilivyopangwa awali lengo likiwa ni maandalizi kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania bara."

Aidha, Sanga alisema wachezaji waliotemwa kwenye usajili kwa ajili ya mzunguko wa pili wameachwa kwa mapendekezo ya kocha huyo.



"Uongozi umepokea mapendekezo ya kocha kwa ajili ya wachezaji wa kuachwa na sisi tunamsikiliza yeye hivyo kocha ndiye anayejua nani wa kuachwa," .

Mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Bara unatarajiwa kuanza Januari 19 mwakani.

Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 29 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 26 huku Simba ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 23.

No comments:

Post a Comment